DOMINIKA YA 2 MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.66:4
Ee Mungu, nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako wewe Uliye juu kabisa.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayeongoza vyote, mbinguni na duniani, uyasikilize kwa wema maombi ya watu wako, na uzijalie nyakati zetu amani yako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.62:1-5
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa. Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1-3,7-10 (K)3
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,

(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.

2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.(K)

3. Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, (K).

4. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Atawahukumu watu kwa adili. (K)

SOMO 2: 1Kor.12:4-11
Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Yesu aliwaambia akasema:
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu,
Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Yn.2:1-12
Wakati ule, palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. Baada ya hayo akashuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake; wakakaa huko siku si nyingi.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Bikira Maria, Yesu na wafuasi wengine walialikwa arusini Kana, Galilaya. Yesu alishiriki furaha za sherehe hata alisaidia kuongeza furaha za watu kwa kuwaletea divai. Ee Bwana Yesu, ulipohudhuria sherehe za arusi, ulitaka kutuonesha kwamba maisha ya ndoa yanapoanza na arusi ni baraka ya Mungu.

Tunaomba,
1. Utusaidie kutambua kwamba maisha ya ndoa ni msingi na nguzo ya kufanikiwa maishani.

2. Uwasaidie watu wa ndoa kuimarisha ndoa zao kwa kuishi kwa uaminifu.

3. Uzilinde familia zetu katika mafarakano, magomvi na fitina za ndani na za nje.

4. Uwasaidie vijana kuwa na uamuzi na nia thabiti ya kufunga ndoa.

5. Uwafunulie vijana kutambua hatari iliyopo katika mahusiano yaliyo kinyume na Sakramenti ya ndoa; Watambue kwamba kuishi katika unyumba bila Sakramenti ya ndoa ni kinyume na amri zako.

6. Uwasaidie wanandoa kutambua kwamba wanakosa kutimiza wajibu wao wanapoziacha familia zao bila msaada.

7. Ubariki familia zote ambazo zinaendelea katika njia ya imani na uaminifu ingawa wanakabiliwa na matatizo mengi.

Ee Mungu Mwenyezi, ulifanya ndoa kuwa msingi wa maisha ya familia bora. Uyapokee maombi yetu kwa njia ya Kristo, Bwana wetu aliyetuwekea sakramenti ya ndoa takatifu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie kushiriki kwa heshima mafumbo haya, kwani, kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.23:5
Waandaa meza mbele yangu, na kikombe changu kinafurika.

AU: 1Yoh.4:16
Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, umimine Roho wa upendo wako ndani yetu, ili sisi uliotushibisha kwa mkate mmoja wa mbinguni, utufanya kuwa moyo mmoja katika upendo mmoja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.