DOMINIKA YA 30 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.105:3-4
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake. Utafuteni uso wake siku zote.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, utuongezee imani, matumaini na mapendo. Utuwezeshe kuyapenda unayoamuru, ili tustahili kupokea unayoahidi. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Yer.31:7-9
Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.126(K)3
1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.

(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

2. Ndipo mataifa waliposema,
Bwana amewatendea mambo makuu,
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)

3. Ee, Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)

4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)

SOMO 2: Ebr.5:1-6
Ndugu, kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.

SHANGILIO: Ef.1:17-18
Aleluya, aleluya!
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uyatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya!

INJILI: Mk.10:46-52
Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, Imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Kipofu alimwendea Yesu akamwomba amrudishie kuona. Yesu akamsikiliza akamwondolea upofu wake.

Ee Baba Mungu,
1. Utufumbue macho ya imani ili tukutambue wewe katika mambo ya kawaida na kukufuata. Ee Bwana.

2. Mambo mengi ya dunia yanatupofusha tusikuone na kukutambua kama Mungu katika matukio ya maisha: Utue neema tukutambue wewe kama Mungu katika matukio ya maisha yetu ya kawaida. Ee Bwana.

3. Utupe neema tuelewe kuwa unatuongoza maishani kwa baraka zako. Ee Bwana.

4. Mambo mengi yanajaribu kuzima imani yetu: Utuamshe tung'amue hatari na vishawishi vinavyotaka kututenganisha nawe. Ee Bwana.

5. Uwaite vijana wengi kufanya kazi ya kuwashirikisha wote habari njema ya wokovu. Ee Bwana.

Ee Mungu Mwenyezi, ulimtuma Mwana wako wa pekee atuondolee upofu wa mioyo yetu. Usikilize maombi yetu tupate kukuona wewe katika Mwana wako, Bwana wetu Yesu Kristo. Amina

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uviangalie vipaji tunavyokutolea wewe mwenye enzi, ili tunayoyatenda katika utumishi wetu, yawe hasa kwa ajili ya utukufu wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.20:5
Tuushangilie wokovu wako, kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu.

Au:
Efe.5:2

Kristo ametupenda, akajitoa kwa ajili yetu sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti zako zitimize ndani yetu yale zinayomaanisha, ili hayo tuyatendayo sasa katika mafumbo, tuyafahamu katika ukweli wake. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.