DOMINIKA YA 31 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.38:21-22
Wewe, Bwana, usiniache; Mungu wangu, usijitenge nami. Ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, nguvu za
wokovu wangu.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na rahimu, kwa neema yako waamini huweza kukutumikia kwa namna inayofaa na ya
kusifika. Tunakuomba utujalie tuweze kuzikimbilia ahadi zako bila kujikwaa. Kwa njia ya
Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
milele na milele.
SOMO 1: Kumb.6:2-6
Musa aliwaambia makutano: Upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria
zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku
zako ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka
sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza,
Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako
wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa
katika moyo wako.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.18:1-3,46,50(K)1
1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu,
Na boma langu na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayekukimbilia.
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu,
Na ngome yangu.
Nitamwita Bwana anayestahili kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
(K) Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana.
2. Bwana ndiye aliye hai,
Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu
Ampa mfalme wake wokovu mkuu,
Amfanyia fadhili masihi wake. (K)
SOMO 2: Ebr.7:23-28
Wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na watu wasikae; bali yeye, kwa kuwa
akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao
wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai siku zote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani
mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengewa na
wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu
wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao
hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu
walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka
Mwana, aliyekamilika hata milele.
SHANGILIO: Yn.15:28-34
Aleluya, aleluya!
Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa baba yangu nimewaarifu.
Aleluya!
INJILI: Mk.12:28-34
Wakati ule, mmojawapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa
amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza
ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja, nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo
wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo
hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi
akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye;
na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama
nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba
amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili
neno tena tokea hapo.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Amri ya kwanza katika imani yetu ni
kumpenda Mungu kwa nguvu zetu zote; amri ya pili ni kumtendea
mwenzetu kama tunavyotaka kutendewa sisi wenyewe.
Ee Baba Mungu,
1. Kukupenda wewe kwa nguvu zetu zote ni kukuabudu wewe peke
yako: Utuimarishe kuweka moyo, akili na roho zetu
kwa ajili ya utumishi kwa wengine. Ee Bwana.
2. Kukupenda wewe kwa moyo wote kwa kushika amri zako ni
kufanikisha maisha yetu: uamshe akili yetu tukutegemee
wewe katika yote. Ee Bwana.
3. Mioyo ni geugeu; Kanisani tunakuheshimu kwa ibada na
uchaji, lakini maishani tunakusahau wewe kama Mungu Muumbaji
wetu: Ufanye maisha yetu ya kila siku yaoneshe imani yetu.
Ee Bwana.
4. Utuongoze tusitafute wokovu wetu mahali pasipopatikana
bali katika wewe. Ee Bwana.
Mungu wa upendo, ulitupa amri ya
kupendana na kwa njia hiyo kujitayarisha kwa maisha ya huko
mbinguni. Usikilize maombi yetu tunayokupelekea kwa jina
la Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunaomba dhabihu hii iwe sadaka safi mbele yako, na ituletee zawadi takatifu ya huruma
yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.16:11
Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako ziko furaha tele, ee Bwana
Au:
Yn.6:57
Bwana asema: Kama vile Baba, aliye hai, alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika
naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba uweza wako uzidi kutenda kazi ndani yetu, ili, baada ya kulishwa sakramenti
ya mbinguni, kwa neema yako tuandaliwe kupokea yaliyoahidiwa na sakramenti hiyo. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.