DOMINIKA YA 32 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.88:2
Maombi yangu yafike mbele zako, uutegee ukelele wangu sikio lako, ee Bwana.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na rahimu, utuepushe kwa radhi yako na yote yawezayo kutudhuru, ili, tukiwa huru rohoni na mwilini, tupate kuyatimiza mapenzi yako pasipo kizuio. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 1Fal.17:10-16
Eliya aliondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:6-10(K)1
1. Bwana huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula;
Naye huwafungua waliofungwa.

(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

2. Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Naye huwainua walioinama.
Bwana huwapenda wenye haki,
Naam, huwahifadhi wageni. (K)

3. Bwana huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)

SOMO 2: Ebr.9:24-28
Kristu hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.

SHANGILIO: Yn.14:6
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!

INJILI: Mk.12:38-44
Yesu aliwaambia katika mafundisho yake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa. Naye akaketi kuielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Bwana Yesu aliketi karibu na sanduku la mchango na kuwatazama waumini Wayahudi waliotoa zaka zao. Mjane aliyetoa fedha yote aliyokuwa nayo alisifiwa na Yesu.

Ee Mungu Baba yetu,
1. Ufungue mioyo yetu tuwe tayari kutoa misaada na zaka kwa moyo mkarimu. Ee Bwana.

2. Ikiwa tunakuheshimu wewe kweli, hatuwezi kukupa kitu hafifu: Utupe moyo wa kukupa wewe heshima unayostahili kama Mungu. Ee Bwana.

3. Ikiwa tunatoa kitu kwa mkono wa kulia, mkono wetu wa kushoto usijue. Utusaidie kutojitafutia sifa kwa michango yetu katika nafasi mbalimbali. Ee Bwana.

4. Waumini wa kwanza wa Yerusalemu walishirikiana katika yote ili kufanikisha umoja wa jamii ya waumini: Utupe neema ya kuiga ari ya wakristo wa kwanza katika ushirikiano wa hali na mali. Ee Bwana.

Ee Mungu Mwenyezi, ulitaka sisi sote tuwe na umoja kati yetu na kusaidiana katika shida zinazowasonga wenzetu. Uyapokee maombi yetiu, kwa Kristo Bwanu wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kuitazama dhabihu hii tunayokutolea, ili, lile tunaloadhimisha katika fumbo la mateso ya Mwanao, tulipokee kwa upendo na uchaji. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.23:1-2
Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza.

Au:
Lk.24:35

Wafuasi walimtambua Bwana Yesu katika kuumega mkate.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kulishwa kipaji kitakatifu, tunakutolea shukrani na kukuomba sana huruma yako. Na kwa kumiminiwa Roho wako Mtakatifu, wale ambao wamepokea nguvu ya mbinguni, wadumu katika neema ya uaminifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.