JUMAPILI YA 33 MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Yer.29:11,12,14
Bwana asema: Mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Nanyi mtaniita nami nitawasikiliza, nami nitawarudisha kutoka mahali pote watu wenu waliofungwa.

KOLEKTA:
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kukutumikia, maana kama tukikutumikia wewe uliye muumba wa mema yote, tunayo heri iliyo kamili siku zote. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Dan.12:1-3
Wakati ule Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja ataonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi hutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:5,8-11(K)1
1. Bwana ndiye fungu la posho langu,
Wewe unaishika kura yangu.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.

(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe.

2. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutaiacha nafsi yangu kuzimu,
Wala hutamto mtakatifu wako aone uharibifu. (K)

3. Utanijulisha njia ya uzima,
Mbele ya uso wako ziko furaha tele.
Na katika mkono wako wa kuume,
Mna mema ya milele. (K)

SOMO 2: Ebr.10:11-14,18
Kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.

SHANGILIO: Ufu.2:10
Aleluya, aleluya!
Uwe mwaminifu hata kufa, asema Bwana; Nami nitakupa taji ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Mk.13:24-32
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu. Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie ili vipaji tulivyotoa mbele ya macho yako wewe uliye mtukufu, vitupatie neema ya kukutumikia kwa uchaji na tunda la heri ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.73:28
Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; nimefanya kimbilio kwa Bwana Mungu.

Au:
Mk.11:23-24

Bwana asema: Amin, nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea mapaji ya fumbo hili takatifu. Tunakusihi kwa unyenyekevu, ili, yale ambayo Mwanao alituagiza kwa ukumbusho wake, yatufae kwa kutuongezea mapendo yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.