JUMAPILI YA 2 BAADA YA NOEL

ANTIFONA YA KUINGIA: Hek.18:14-15
Majira mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno wako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, mwangaza wa mioyo ya waamini, tunakuomba ukubali kwa wema kuujaza ulimwengu utukufu wako, nawe uonekane kwa mataifa yote kwa nuru ya mwanga wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Ybs.24:1-2,8-12
Hekima atajisifu nafsi yake, na katikati ya watu wake atajiadhimisha; katika mkutano wake aliye juu atafumbua kinywa chake, na kujitukuza mbele ya majeshi yake. Ndipo Muumba vitu vyote aliponiagiza, Aliyeniumba aliisimamisha hema yangu; Akasema, Maskani yako iwe katika Yakobo, Urithi wako na uwe katika Israeli. Tangu awali aliniumba kabla ya ulimwengu, Wala sikomi kabisa hata milele. Katika hema takatifu nikahudumu mbele zake, Vivyo hivyo nikathibitika katika Sayuni, Katika mji upendwao akanistarehesha, Na katika Yerusalemu nikapewa amri; Nikatia shina katika Taifa lililo tukufu, Naam, katika sehemu ya urithi wa Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.147:12-15,19-20(K)Yn1:1
1. Msifu Bwana, ee Yerusalemu
Msifu Mungu wako, ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.

(K) Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.
Au: Aleluya.

2. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

SOMO 2: Efe.1:3-6,15-18
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na Uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo.

SHANGILIO: Tim.3:16
Aleluya, aleluya!
Sifa kwako, ee Kristo, unayehubiriwa katika mataifa.
Sifa kwako, ee Kristo, unayeaminiwa katika ulimwengu.
Aleluya!

INJILI: Yn.1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, Naye Neno alikuwako kwa Mungu, Naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu, Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu, Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohane alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba vipaji tunavyokutolea uvitakase kwa kuzaliwa kwake Mwanao pekee, kunakotuonesha njia ya ukweli na kutuahidi uzima wa ufalme wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI wa Kuzaliwa kwa Bwana. I, II au III.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.1:12
Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba kwa unyenyekevu dhambi zetu zitakaswe kwa nguvu ya sakramenti hii, na nia zetu njema zitimizwe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.