DOMINIKA YA 3 MAJILIO
MASOMO MWAKA C
ANTIFONA YA KUINGIA: Flp.4:4-5
Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu.
KOLEKTA
Ee Mungu, unatuona sisi taifa lako tukiingojea Kiaminifu sherehe ya kuzaliwa kwake Bwana wetu.
Tunakuomba utujalie tuweze kuzifikia furaha za wokovu huo mkubwa sana, na kuziadhimisha daima kwa
ibada kuu na shangwe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika
umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Sef.3:14-18
Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti
Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana,
yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono
yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu,
Atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada,
hao waliokuwa wa kwako.
WIMBO WA KATIKATI: Isa.12:2-6(K)6
1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu.
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu.
(K) Paza sauti, piga kelele
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
2. Mshukuruni Bwana, liiteni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
3. Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)
SOMO 2: Flp.4:4-7
Ndugu zangu: Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote.
Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na
kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo
yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
SHANGILIO: Lk.4:18
Aleluya, aleluya!
Roho wa Bwana yu juu yangu,
Amenituma kuwahubiri maskini habari njema;
Aleluya!
SOMO 3: INJILI: Lk.3:10-18
Siku ile: Makutano wakamwuliza Yohane Mbatizaji, Tufanye nini basi? Akawajibu akawaambia, Mwenye kanzu
mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa,
wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari onao
wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo;
tena mtoshewe na mshahara wenu. Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni
mwao habari za Yohane, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza
kwa maji; lakini anakuja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu
vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye
atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto
usiozimika. Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu katika Kristo, kwa imani na matumaini tumwombe sasa Mungu msaada wake
Tukiitikia. "Bwana utuhurumie - Bwana utuhurumie".
1. Kwa ajili ya Kanisa: Ee Baba Mungu Mwenyezi tunakuomba, ulikamilishe Kanisa lako na kulifanya ishara
wazi kwa watu wote.
2. Kwa ajili ya ulimwengu: Ee Mungu Mwenyezi, utengeneze upya ulimwengu huu kwa kuupatia haki na amani ili
Mwanao apate mahali pazuri pa kufikia.
3. Kwa ajili ya watu wote wasio na matumaini: Tunakuomba Ee Baba Mwenyezi, uwaangaze wale wote wasio na
imani bado ili wapate kumtambua Mwanao na kumsadiki kama Mkombozi wao.
4. Kwa ajili yetu sisi tuliokusanyika hapa: Ee Mungu Mwenyezi tunakuomba, ututakase sisi tuliopo hapa,
uimarishe imani yetu ili tungojee kwa matumaini makubwa ujio wa pili wa Mkombozi wetu Yesu Kristo.
5. Kwa ajili ya watu wote: uwasadikishe watu wote wakusadiki na kuamini kuwa bila Yesu Kristo hakuna
Wokovu.
6. Kwa ajili ya marehemu wote: Ee Baba Mungu Mwenyezi, wahurumie na kuwatakasa marehemu wetu wote na
kuwapa raha ya milele.
Ee Mungu Baba yetu, unayetia nguvu ndani ya mioyo iliyolegea, upokee kwa huruma maombi yetu tuwe imara
daima, kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba sadaka ya ibada yetu itolewe kwako daima. Nayo itimize agizo la
kuadhimisha fumbo takatifu, na kutenda kwa mafanikio wokovu wako ndani yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.
1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu,
tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele,
kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu
wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa
milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema
yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja
na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni,
twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:
W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.35:4
Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wetu atakuja na kutuokoa.
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tunakuomba utujalie huruma yako, ili misaada hii ya kimungu ituondolee dhambi zetu, na kutuweka
tayari kwa sikukuu zijazo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.