DOMINIKA YA 3 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.96:1,6
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana, nchi yote. Heshima na adhama zimo mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, uelekeze mwenendo wetu kadiri ya mapenzi yako, ili kwa jina la Mwanao mpendwa tustahili kujaa matendo mema. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu milele na milele.

SOMO 1: Neh.8:1-10
Watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, Bwana aliyowaamuru Israeli. Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha torati. Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:7-9,14 (K)Yoh.6:63
1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.

(K) Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu;
maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.

2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)

3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

4. Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)

SOMO 2: 1Kor.12:12-30
Kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?

SHANGILIO: Lk.4:18-19
Aleluya, aleluya!
Bwana amenituma, kuwahubiri maskini habari njema,
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,
Aleluya!

INJILI: Lk.1:1-4,4:14-21
Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa. Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Bwana Yesu alipoanza kazi hadharani alitangaza msamaha mkubwa wa Mungu Baba. Hivyo kwa njia ya Yesu wote wanajaliwa Msamaha na kupewa mwanzo mpya wa maisha ya kiimani. Ee Mungu Mwenyezi, Mwana wako wa pekee alifika duniani ili kutujalia msamaha wako,

1. Uhimize mioyo yetu kuitikia na kupokea msamaha wako na kubadili maisha yetu yaendane na amri zako.

2. Utuangaze tutambue kwamba kuishi katika msamaha ni bora zaidi kuliko kuishi katika utumwa wa dhambi.

3. Ututie moyo wa kutambua dhambi zetu na kukurudia kwa njia ya sakramenti ya Upatanisho.

4. Utusaidie kutambua kwamba maisha bila Wewe huleta hasara, na kwamba maisha pamoja nawe huleta mafanikio.

5. Ujaze mioyo yetu furaha ya kumfuata Yesu kama kiongozi wa maisha yetu.

Ee Mungu Baba, tunatambua kwamba maisha bila kutegemea msamaha wako, ni bure. Bila mwanga wako tunapotea katika giza la ubaya na maovu. Utusaidie kumwendea Mwana wako Bwana wetu, Yesu Kristu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, upende kuvipokea kwa wema vipaji vyetu. Tunakuomba uvitakase, uvifanye viwe kwetu chemchemi ya wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:5
Walimwelekea Bwana macho wakatiwa nuru, wala nyuso zao hazitaona haya.

AU: Yn.8:12
Bwana asema: Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba utujalie ili, kwa kuipokea neema iletayo uzima wako, tuone daima fahari juu ya fadhili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.