JUMAPILI YA 4 KWARESIMA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.66:10-11
Furahi, ee Yerusalemu, na mkusanyike, ninyi nyote mmpendao. Furahini kwa furaha, ninyi nyote mliokuwa na huzuni, mpate kushangilia, na kushibishwa kwa utamu wa faraja zake.

KOLEKTA:
Ee Mungu, kwa kazi ya Neno wako unawaletea wanadamu upatanisho kwa namna ya ajabu. Tunakuomba uijalie jamii ya wakristo izidi kuzijongea sikukuu zijazo kwa utayari wa ibada na imani hai. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Yos.5:9a,10-12
Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya Pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-6,(K)8
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima,
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

SOMO 2: 2Kor.5:17-21
Ndugu zangu, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye.

SHANGILIO: Lk.15:18
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia,
Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.

INJILI: Lk.15:1-3,11-32
Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi mwanambuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Mungu wetu si hakimu mkali aliye na nia ya kutoa adhabu tu, bali Yesu alituonesha kuwa Mungu ni Baba mwenye huruma ya kuwapokea na kuwarudisha watoto waliopotea.

Tumwendee Baba yetu wa huruma,
1. Utuoneshe njia nzuri za kuwasaidia na kuwarudisha waliopotea sababu ya mahangaiko na matatizo ya maisha.

2. Uwasaidie wakubwa wa Kanisa wagundue njia na mitindo mizuri ya kuwasaidia waumini walionaswa kwa vishawishi na kuacha imani yao.

3. Utupe sisi moyo wa kutegemea huruma na wema wako wakati tunapogandamizwa kwa dhambi zetu.

4. Utunyoshee mikono yako na kutuokoa tunapozama katika makosa na dhambi.

5. Uwasaidie wazazi kuwapokea watoto wao wanaopotea na kupata shida kwa sababu ya ujinga wao wa kitoto.

6. Utufundishe kutambua kwamba kusameheana kunaweka msingi wa maisha mapya.

Ee Mungu Baba, tunakushukuru kwa sababu Mwana wako alituonesha tabia yako ya kuhurumia. Humwachi mtu yeyote apotee. Utuimarishie imani ili tufurahie huruma yako unayeishi daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakutolea kwa furaha dhabihu iletayo ukombozi wa milele. Tunakuomba kwa unyenyekevu utujalie tuiheshimu kwa moyo mwaminifu na kuitoa inavyofaa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.15:32
Mwanangu, kufanya furaha na shangwe ilipasa,kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa,naye amefufuka; alikuwa amepotea,naye ameonekana.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu, unamtia nuru kila mtu ajaye katika ulimwengu huu. Tunakuomba uziangaze nyoyo zetu kwa nuru ya neema yako, ili tuweze kuwaza daima yaipendezayo adhama yako, na kukupenda wewe kwa dhati. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Bwana, uwalinde wanaokusihi, uwaimarishe walio dhaifu, uwape nguvu siku zote kwa mwanga wako wale wanaotembea katika uvuli wa mauti, na uwaopoe katika maovu yote ili wapate kuyafikia yale mema yapitayo mema yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.