DOMINIKA YA 4 MAJILIO
MASOMO MWAKA C
ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.45:8 Vulg.
Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi.
KOLEKTA
Ee Bwana, tunakuomba utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa ujumbe wa Malaika kwamba Kristo
Mwanao amejifanya mtu, kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Kwa njia ya Bwana
wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na
milele.
SOMO 1: Mik.5:2-4
Bwana asema: wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe
atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale,
tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya
nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi
ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia. Na mtu huyu
atakuwa amani yetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.80:1-2,14-15,17-18 (K)3
1. Wewe uchungaye Israeli usikie,
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako.
Uje, utuokoe.
(K) Ee Mungu, uturudishe,
Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
2. Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya
Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)
3. Mkono wako na uwe juu yake
Mtu wa mkono wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya
Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. (K)
SOMO 2: Ebr.10:5-10
Ndugu zangu: Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, Kristo asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea
tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja
(katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo
na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru
torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi
alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
SHANGILIO: Lk.1:38
Aleluya, aleluya!
Mariamu akasema, tazama mimi ni mjakazi wa Bwana;
na iwe kwangu kama ulivyosema.
Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Aleluya!
SOMO 3: INJILI: Lk.1:39-45
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia
nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti. Ikawa Elizabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto
kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema,
Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili hata mama
wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga
kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa
na Bwana.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Bikira Maria alikwenda kumtazama jamaa yake Elizabeti aliyekuwa mjamzito.
Ee Baba wa huruma,
1. Utupe moyo wa kuwasaidia majirani zetu katika shida zao.
2. Utujalie moyo wa kujitwika kazi, shughuli na matatizo katika kuwahudumia wenzetu kama alivyofanya
Bikira Maria.
3. Uwasaidie wakubwa wetu kukumbuka wajibu wao wa kuwasaidia. wadogo na wanyonge.
4. Uwape akina mama wetu moyo wa kuwatunza watoto wao, kuwalea katika imani na kuwatayarisha kwa maisha
ya siku za mbele.
5. Uwatuze marehemu wetu kwa mema yote waliyowatendea wenzao duniani.
Ee Mungu Baba, sisi tunategemea kusikilizwa nawe kwa maombezi ya Bikira Maria Mtakatifu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, Roho yule ambaye kwa uwezo wake Maria mwenye heri alipata mimba, avitakase vipaji
vyetu tulivyoviweka juu ya altare yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO II:
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru
Wewe daima na popote, ee Bwana Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.
Yeye ambaye alitabiriwa na maaguzi ya manabii wote, Mama Bikira alimchukua kwa upendo
wa ajabu, na Yohane Mbatizaji alishangilia kuja kwake na kumtambulisha alipofika. Yeye aliyetujalia
kungojea kwa furaha fumbo la kuzaliwa kwake, atukute tukikesha katika sala na tukimshangilia kwa
nyimbo za kumsifu.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika wakuu, pamoja na Viti vya
enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema
bila mwisho:
W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.7:14
Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi inavyokaribia hiyo
sikukuu ituleteayo wokovu, hivyo zizidi bidii za ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa
kwake Mwanao. Anayeishi na kutawala milele na milele.