DOMINIKA YA 5 MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.95:6-7
Njoni, tumwabudu Mungu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye
Bwana Mungu wetu.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba, uilinde familia yako kwa wema wako usio na mwisho, ili, hao wanaotegemea
tumaini la neema ya mbinguni tu, waimarishwe daima na ulinzi wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.6:1-2a,3-8
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na
kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa
na mabawa sita. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana
wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti
yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu
mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu
yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa
na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa
kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa,
na dhambi yako, imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ninani
atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.138:1-5,7-8,(K)1
1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
Nitalishukuru jina lako.
(K) Ee Bwana, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
2. Nitalishukuru jina lako,
Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
3. Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru,
Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
Naam, wataziimba njia za Bwana,
Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. (K)
4. Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimilizia mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)
SOMO 2: 1Kor.15:1-11
Ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama,
na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa
maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili
ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama
yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi
ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea
Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa
wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika Mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa
la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure,
bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi,
kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana,
Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!
INJILI: Lk.5:1-11
Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa la
Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.
Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi,
akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini,
mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha
usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata
samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo
cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro
alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi,
Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki
walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia
Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha
vyote wakamfuata.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Bwana Yesu hakuwa mvuvi, kwa hiyo Petro alithubutu
kumkumbusha Yesu kwamba ni kazi bure kuvua samaki mchana.
Hata hivyo alimtii Yesu akashusha nyavu tena baharini.
Ee Mungu Baba, Yesu alitaka kututia moyo wa kumtegemea
kabisa hata katika matatizo makubwa. Yeye yupo katika chombo
chetu kinachoyumbishwa na mawimbi ya maisha. Tunakuomba,
1. Utukumbushe kwamba Yesu, msaada wetu, yupo karibu
nasi, naye yu tayari kabisa kutusaidia tukimwendea hasa
tunapopatwa na matatizo.
2. Utuongezee matumaini tusikate tamaa katika hali yoyote,
bali tumkimbilie Yesu katika mahangaiko yetu.
3. Uwaimarishe wasaidizi katika kazi za uchungaji kutokufa
moyo wanapokabiliwa na matatizo katika kazi zao.
4. Uwaongoze na kuwasaidia mapadre, mashemasi na wote
wanaotoa huduma za kiroho katika kazi zao.
5. Uwaamshe vijana wengi kujiunga na kazi katika Kanisa
lako.
6. Uwape tuzo ya uzima wa milele marehemu wote waliojitoa
katika utumishi wa Kanisa.
Ee Baba wa huruma, mitume walifanikiwa katika kazi zao kwa
nguvu ya Yesu. Utukirimie kwa kutusikiliza maombi yetu kwa njia
ya Kristu, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana Mungu wetu, umeumba vitu hivi ili vitusaidie hasa katika udhaifu wetu. Tunakuomba
utujalie viwe pia sakramenti ya kutuletea uzima wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.1:12
Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, na maajabu yake kwa wanadamu; maana hushibisha nafsi
yenye shauku, na nafsi yenye njaa huijaza mema.
AU: Mt.5:4,6
Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao
watashibishwa.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu, umependa tushiriki mkate mmoja na kikombe kimoja. Tunakuomba utujalie kuishi tumeungana
na Kristo, tupate kuzaa matunda kwa furaha, kwa manufaa ya wokovu wa ulimwengu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.