DOMINIKA YA 6 MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.31:2-3
Ee Mungu, uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, usemaye kuwa unakaa ndani ya mioyo ya walio wema na wanyofu, utujalie ili, kwa neema yako, tupate kuwa makao yako yanayokupendeza. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Yer.17:5-8
Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani. Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jina lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6,(K)40:4
1. Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake,
Wala hakuwaelekea wenye kiburi.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

SOMO 2: 1Kor.15:12,16-20
Ndugu zangu, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

SHANGILIO: Efe.1:17-18
Aleluya, aleluya!
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya!

INJILI: Lk.6:17,20-26
Yesu alishuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema,
Heri ninyi mlio maskini,
kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.
Heri ninyi mlio na njaa sasa,
kwa sababu mtashiba.
Heri ninyi mliao sasa,
kwa sababu mtacheka.
Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.
Furahiwani siku ile na kurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo.
Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali,
kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata.
Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa,
kwa kuwa mtaona njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
kwa kuwa mtaomboleza na kulia.
Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu,
kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Yesu alipoanza kutangaza habari njema ya wokovu, hakuanza kwa kulaumu wala kukaripia, bali alitangaza heri za ufalme wa Mungu. Ee Bwana Yesu,

1. Utuzibue masikio yetu ya kiroho ili ahadi zako zipenye mioyo yetu iliyonaswa katika shughuli za kidunia.

2. Utusaidie kuamini kwamba mali ya dunia hii haiwezi kutupatia heri na furaha ya kweli.

3. Utujalie kutambua kwamba tunajiwekea hazina kwako tunapotenda matendo ya huruma, wema na upendo.

4. Utukumbushe kutambua kwamba tunaweza kuangaza maisha ya wenzetu na kuyafanya mazuri zaidi kwa kuwashirikisha mali yetu, vipaji vyetu na upendo wetu.

5. Utuoneshe njia za kuleta furaha ya kweli duniani badala ya uchungu, hasira na wivu kwa kujitafutia faida ya binafsi.

6. Utusaidie kutambua kwamba tuna wajibu mkubwa wa kutunza amani ili dunia iwe na amani na usalama.

Ee Mungu wa huruma, toka mwanzo ulitaka tupate heri badala ya mateso. Uyasikilize maombi yetu ambayo tunapeleka kwako kwa njia ya Mwana wako aliyetutangazia heri hiyo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba ili matoleo ya sadaka hii yatutakase na kutufanya wapya; tena kwa wale wanaotimiza mapenzi yako yawe sababu ya kupata thawabu ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.78:29-30
Wakala, wakashiba sana, maana Bwana aliwaletea walivyovitamani; hawakuachana na matakwa yao.

AU: Yn.3:16
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kula chakula cha mbinguni, tunakuomba tutamani daima chakula hicho kilicho kwetu chemchemi halisi ya uzima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu