DOMINIKA YA 7 MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.13:6
Nami nimezitumainia fadhili zako; moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie Bwana, kwa
kuwa amenitendea kwa ukarimu.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba utujalie tutafakari daima yaliyo mema, ili tutimize kwa maneno na matendo
yale yanayokupendeza. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja
wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: 1Sam.26:2,7-9,12-13,22-23
Sauli aliondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja
naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama,
Sauli alikuwepo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake;
naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako
mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili.
Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masiya
wa Bwana, naye akawa hana hatia?" Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji kichwani pa
Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili, wala kulijua, wala kuamka; maana wote
walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng'ambo
ya pili, akasimama juu ya kilima mbali sana; palikuwapo nafasi tele katikati yao. Daudi akajibu, akasema,
“Litazame fumo hili, ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae. Naye Bwana atamlipa kila mtu haki
yake, na uaminifu wake; maana Bwana amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyosha mkono wangu
juu ya masiya wa Bwana.”
WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,8,10,12-13 (K)8
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana;
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
2. Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema, (K)
3. Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)
4. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. (K)
SOMO 2: 1Kor.15:45-49
Ndugu zangu, ndivyo ilivyoandikwa: Mtu [wa kwanza, Adamu,] akawa nafsi iliyo hai. Adamu wa mwisho
ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.
Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo,
ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.
Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
SHANGILIO: Yn.13:34
Aleluya, aleluya!
Nawapa amri mpya, mpendane.
Kama vile nilivyowapenda ninyi,
Nanyi mpendane vivyo hivyo.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:27-38
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni
mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea
ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho lako, usimzuilie na kanzu. Mpe
kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee
ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonesha fadhili gani? Kwa kuwa
hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonesha
fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu
kwao, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vilevile. Bali
wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi;
nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma,
kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni,
nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata
kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kilekile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Katika Injili ya leo tumesikia kanuni kuu ya maisha yetu: Jinsi
mnavyopenda kutendewa na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.
Ee Mungu Baba,
1. Utufundishe kuacha kulipiza kisasi bali tuishi kwa
uelewano na ushirikiano.
2. Utuwezeshe kuwapenda na kuwabariki wale wanaotukosea.
3. Ulainishe mioyo yetu, tutafute njia ya kupatanishwa badala
ya kutunza uchungu, chuki na hasira mioyoni mwetu.
4. Utusaidie kutambua kwamba wema na upole hutusaidia
kuishi kwa amani.
5. Utuondoshee choyo na kutufanya wakarimu, kwa kuwa
umetuahidia kwamba utaturudishia thawabu kwa kipimo
chema kilichoshindiliwa.
6. Uwakarimie marehemu wote walioonesha ukarimu kwa
wengine.
Ee Mungu Baba, amri yako ni rahisi kutimiza kwa kuwa hatuhitaji
silaha wala vyombo ila moyo wa kupenda tu. Uyapokee maombi
yetu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu aliyetuambia kwamba
Wewe, Baba, ni upendo, daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, sisi tunaoadhimisha mafumbo yako ipasavyo, tunakuomba sana, hayo tunayokutolea kwa
heshima ya utukufu wako yatufae kwa wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.9:1-2
Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kukushangilia Wewe; nitaliimbia jina
lako, Wewe Uliye juu.
Au: Yn.11:27
Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba utujalie mapato ya wokovu, ambao amana yake tumeipata kwa mafumbo
haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.