DOMINIKA YA 8 MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Taz.Zab 18:18-19
Bwana alikuwa tegemeo langu, akanitoa akanipeleka panapo nafasi, akaniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba uyaongoze mambo ya ulimwengu yafuate utaratibu wako ili tuwe na amani; na Kanisa
lako lifurahie kukuabudu kwa utulivu. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: YbS.27:4-7
Kutikisa chekecheke, itabaki wishwa; Vilevile ila za mtu katika kujadili. Tanuu hujaribu vyombo vya mfinyanzi;
Vilevile jaribio la mtu ni kujadili. Matunda ya mti huonesha ulimaji wake; Vilevile kujadili mawazo ya moyoni.
Usimsifu mtu usijemsikia anajadili; Hakika hilo ni jaribio la wanadamu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.92:1-2,12-15,(K)1
1. Ni neno jema kumshukuru Bwana,
Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.
Kuzitangaza rehema zako asubuhi,
Na uaminifu wako wakati wa usiku.
(K) Ni neno jema kumshukuru Bwana.
2. Mwenye haki atastawi kama mtende,
Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
Waliopandwa katika nyumba ya Bwana
Watasitawi katika nyua za Mungu wetu. (K)
3. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili,
Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu. (K)
SOMO 2: 1Kor.15:54-58
Wapenzi, uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa
lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, ewe mauti,
uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye
kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana
kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.
SHANGILIO: Mt.4:23
Aleluya, aleluya!
Kristo alihubiri habari njema ya ufalme
na kuponya wagonjwa na udhaifu
wa kila namna katika watu.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:39-45
Yesu aliwaambia mithali, Je, aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?
Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake.
Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho
lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho
ndani ya jicho lako, nawe huangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? itoe kwanza ile boriti
katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu
yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila
mti hutambulika kwa matunda yake; maana katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi
zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu
ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ee Bwana, tunakiri kwamba tunaona zaidi kibanzi katika jicho la
mwenzetu kuliko boriti katika jicho letu, kwa kuwa tunataka
kufunua makosa ya wenzetu ili kuficha makosa yetu. Lakini
ulituambia: msihukumu msije mkahukumiwa.
Tunaomba,
1. Kwa ajili ya Kanisa letu: Roho wako aliongoze Kanisa
kutafuta umoja wa Waristo wote bila kushtakiana kwa
sababu ya makosa ya zamani.
2. Kwa ajili ya mataifa ya dunia: Uyajalie amani, ili watu
wote waishi katika hali ya kufaa kwa maisha yao.
3. Kwa ajili ya waumini wenzetu: Uwaangaze watambue
kwamba wanaweza kujenga umoja katika parokia yetu kwa
bidii ya kushirikiana katika kazi ya uchungaji.
4. Utupe sisi sote roho ya uelewano na kupendana badala ya
kutafutiana makosa na kugombana.
Ee Mungu Mwenyezi, hatuwezi kutoa matunda mazuri bila msaada
wako. Kwa hiyo ututimilizie maombi yetu kwa Kristo Bwana
wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, wewe unatupatia vitu hivi vya kukutolea kwa heshima ya jina lako, na kuvihesabu kuwa
sadaka ya ibada yetu ya kukutumikia. Tunakuomba rehema yako, ili hayo unayotujalia kusudi yatuletee
mastahili, yatufae pia kupata tuzo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.13:6;7:17
Naam, nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu; nitaliimbia jina la Bwana Aliye juu.
Au: Mt.28:20
Tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari, asema Bwana.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kushiba kipawa kiletacho wokovu, tunakusihi utupe rehema yako, ili sakramenti
hii unayotulisha hapa duniani itufanye tuwe washiriki wa uzima wa milele kwa hisani yako. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu.