Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 12 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Mfanyieni Mungu shangwe, dunia yote: mtumikieni Bwana kwa furaha.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Kwa kuwa sasa jua laangaza,
Nyoyo zetu kwa Mungu twainua,
Atuepushe na maovu leo
Katika yote matendo, maneno.

Atuepushe na ubishi wa bure,
Atukinge na chuki na hasira;
Yasiyofaa tusiyatazame,
Na ya upuzi tusiyasikie.

Adumishe safi dhamiri zetu,
Ya kijinga na tusiyafuate;
Atuwezeshe kujikatalia,
Na majivuno yetu kuzuia.

Ili, siku hii itakapokwisha,
Na usiku kuingia ukisha,
Kwa ushindi tusifu lake Jina,
Kwa dhamiri zisizo na mawaa.

ANT. I: Moyo wangu u tayari, Ee Mungu, moyo wangu u tayari.

Zab.108 Sala ya kujiunga na maadui
Kwa kuwa Mwana wa Mungu ametukuzwa juu ya mbingu, utukufu wake hutangazwa duniani kote (Arnobius)

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;/
nitaimba na kukushangilia!*
Amka, ee roho yangu!

Amkeni enyi zeze na kinubi;*
nitayaamsha mapambazuko!

Ee Mungu, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu wafika juu ya mbingu;*
uaminifu wako waenea hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;*
utukufu wako uenee duniani kote.

Uwasalimishe hao watu uwapendao;*
utuokoe kwa mkono wako, na kutusikiliza.

Mungu amesema kutoka patakatifu pake;/
"Sasa nitakwenda kwa shangwe kuigawa Shekemu;*
bonde la Sukoti nitaligawa sehemu sehemu.

Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu;/
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,*
na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.

Moabu ni kama bakuli langu la kunawia;/
kiatu changu nitaweka juu ya Edomu, kuimiliki,*
nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia!”

Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wenye ngome?*
Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?

Je, umetuacha kabisa, Ee Mungu?*
Je, huendi tena na majeshi yetu?

Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu,*
maana msaada wa binadamu haufai kitu.

Tutashinda, Mungu akiwa upande wetu,*
yeye atawaponda adui zetu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Moyo wangu u tayari, Ee Mungu, moyo wangu u tayari.

ANT. II: Bwana amenivika vazi la haki na wokovu.

WIMBO: Isa.61:10-62:5 Nabii hufurahia Yerusalemu mpya
Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ... umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa, tayari kukutana na mumewe (Ufu.21:2)

Nitafurahi sana katika BWANA,*
nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu;

maana amenivika mavazi ya wokovu,*
amenifunika vazi la haki,

kama bwana arusi ajipambavyo*
kwa kilemba cha maua,

na kama bibi arusi ajipambavyo*
kwa vyombo vya dhahabu.

Maana kama nchi itoavyo machipuko yake,/
na kama bustani ioteshavyo vitu*
vilivyopandwa ndani yake,

ndivyo BWANA MUNGU atakavyootesha haki na sifa*
mbele ya mataifa yote.

Kwa ajili ya Sion sitanyamaza,*
na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,

hata haki yake itakapotokea kama mwangaza,*
na wokovu wake kama taa iwakayo.

Na mataifa wataiona haki yao*
na wafalme wote watauona utukufu wako;

nawe utaitwa jina jipya,*
litakalotajwa na kinywa cha BWANA.

Nawe utakuwa taji ya uzuri*
katika mkono wa BWANA,

na kilemba cha kifalme*
mkononi mwa Mungu wako.

Hutaitwa tena Aliyeachwa,*
wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa;

bali utaitwa "Namfurahia,"*
na nchi yako "Aliyeolewa;"

kwa kuwa BWANA anakufurahia,*
na nchi yako itaolewa.

Maana kama vile kijana*
amwoavyo mwanamwali,

ndivyo wana wako*
watakavyokuoa wewe;

na kama vile bwana arusi*
amfurahiavyo bibi arusi,

ndivyo Mungu wako*
atakavyokufurahia wewe.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana amenivika vazi la haki na wokovu.

ANT. III: Nitamsifu Mungu wangu, siku zote za maisha yangu.

Zab.146 Sifa kwa Mungu Mkombozi
Na tumtukuze Bwana siku zetu zote, yaani katika matendo yetu yote (Arnobius)

Ee nafsi yangu, umsifu Mungu!/
Nitamsifu Mungu maisha yangu yote;*
nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.

Msiwategemee wakuu wa dunia;*
hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa.

Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho,/
anarudi mavumbini alimotoka;*
na hapo mipango yake yote hutoweka.

Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo,*
mtu ambaye anamtegemea Mungu, Mungu wake,

aliyeumba mbingu na dunia,/
bahari na vyote vilivyomo.*
Yeye hushika ahadi yake milele.

Huwapatia wanaoonewa haki zao,*
na kuwapa wenye njaa chakula.

Mungu huwapa wafungwa uhuru,*
huwafungua macho vipofu.

Mungu huwainua waliokandamizwa,*
huwapenda watu walio waadilifu.

Mungu huwalinda wageni,/
huwategemeza wajane na yatima;*
lakini huangamiza mwenendo wa waovu.

Mungu atawala milele,*
Mungu wako, ee Sion, ni mfalme kwa vizazi vyote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Nitamsifu Mungu wangu, siku zote za maisha yangu.

SOMO: Kum.4:39-40a
Ujue leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa BWANA ndiye Mungu katika mbingu juu na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo.

KIITIKIZANO
K. Nitamtukuza Bwana nyakati zote. (W. Warudie)
K. Sifa yake itakuwa siku zote midomoni pangu.
W. Nyakati zote nitamtukuza.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Nitamtukuza...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Tumtumikie Bwana kwa utakatifu, siku zote za maisha yetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tumtumikie Bwana kwa utakatifu, siku zote za maisha yetu.

MAOMBI
Atukuzwe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa huruma yake kuu, alitufanya tuzaliwe upya na akatujalia tumaini la uzima, kwa njia ya ufufuko wa Mwanae. Tuombe:
W. Baba, utujalie nguvu zako.

Yaelekeze macho yetu kwa Yesu Kristo, Mwanao.
- Atuongoze katika imani yetu, na aikamilishe imani hiyo. (W.)

Utujalie moyo wa furaha na ukarimu;
- ili tulete furaha majumbani mwetu, kazini na kwa wote tunaokutana nao. (W.)

Tunawaombea wakulima na wafanyakazi wote;
- uwe pamoja nao vijijini na mijini, mashambani, viwandani na ofisini. (W.)

Twakuomba uwasaidie wote wasioajiriwa;
- pia uwasaidie walemavu, wagonjwa na wale waliostaafu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, ulikumbuke agano lako takatifu, ulilolifanya upya na kulibariki kwa damu ya Mwana-Kondoo, ili watu wako wapate msamaha wa dhambi zao, na wadumu katika neema zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.