Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 12 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe Utatu, Nuru tukufu,
Ewe Umoja, Wa enzi kuu,
Jua 'mezama, Basi chomoza
Yako mionzi, Mwetu nyoyoni.

Twakutolea, Wimbo wa sifa
Asubuhi, na, Jioni sala;
Pamwe maombi, Twasifu sana
Yako adhama, Milele yote.

ANT. I: Bwana, jinsi ulivyo wa ajabu ujuzi huu wako, ulinidhihirishia!

Zab.139:1-18,23-24 Mungu ajua yote, aongoza yote
Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake? (Rom.11:34)

I
Ee Mungu, wewe umenipima,*
na wanijua mpaka ndani.

Nikiketi au nikisimama, wewe wajua;*
wewe wajua kila kitu ninachonuia.

Nikiwa kazini au nikipumzika, wewe waniona;*
wewe wazijua shughuli zangu zote.

Kabla sijasema neno lolote,*
wewe, Ee Mungu, umekwisha jua yote.

Wanizunguka kila upande,*
waniwekea mkono wako kunilinda.

Maarifa yako yapita akili yangu,*
ni makuu mno, siwezi kuyaelewa.

Nikimbilie wapi mbali nawe?*
Niende wapi ambako wewe hupo?

Nikipanda juu mbinguni, wewe upo;*
nikijilaza chini kuzimu, wewe upo.

Nikiruka hata huko jua linakochomoza,*
au hata mipakani mwa bahari,

hata huko utanikuta;*
mkono wako wa kulia utaniongoza.

Kama ningeliomba giza linifunike,*
na badala ya mwanga usiku unizunguke,

kwako giza si giza hata kidogo,/
na usiku wang'ara kama mchana;*
kwako giza na mwanga ni mamoja.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, jinsi ulivyo wa ajabu ujuzi huu wako, ulionidhihirishia!

ANT. II: Mimi ni Bwana, ambaye hujaribu mawazo na mioyo; nampa kila mtu kile anachostahili kwa matendo yake.

II
Wewe umeniumba mwili na roho;*
ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu.

Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu,/
matendo yako ni ya ajabu;*
natambua jambo hilo kwa moyo wangu wote.

Nilipokuwa naumbwa kwa siri,/
natengenezwa ndani ya ardhi,*
wewe ulinijua kinaganaga.

Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa,*
uliandika kila kitu kitabuni mwako;

siku zangu zote uliziandika,*
hata kabla ya kuweko ile ya kwanza.

Ee Mungu, ni vigumu mno kuyaelewa mawazo yako;*
hayawezi kabisa kuhesabika.

Kama nisivyoweza kuhesabu mchanga,*
ndivyo nisivyoweza kuyahesabu;

na hata kama ningeweza,*
bado wewe ungekuwa pamoja nami.

Unichunguze, Ee Mungu, uujue moyo wangu;*
unipime, uyajue mawazo yangu.

Uangalie nisije nikafuata mwenendo mbaya,*
uniongoze katika njia ya milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mimi ni Bwana, ambaye hujaribu mawazo na mioyo; nampa kila mtu kile anachostahili kwa matendo yake.

ANT. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.

Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu

katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.

Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,

ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.

Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,

vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.

Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.

Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.

Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,

ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.

Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.

Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.

Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,

na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

SOMO: 1Yoh.2:3-6
Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua Mungu. Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi, mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. Lakini mtu ye yote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo wa Mungu kamili ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye: mtu ye yote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.

KIITIKIZANO
K. Utulinde, Ee Bwana, kama mboni ya jicho lako. (W. Warudie)
K. Utufiche kivulini mwa mabawa yako.
W. Ee Bwana, utulinde.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utulinde...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ee Bwana, onesha nguvu za mkono wako; uwashushe wenye kiburi, uwapandishe wanyenyekevu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ee Bwana, onesha nguvu za mkono wako; uwashushe wenye kiburi, uwapandishe wanyenyekevu.

MAOMBI
Tumwombe Baba, atujalie Roho wa Mwanae akae mioyoni mwetu:
W. Baba, kwa huruma yako, utusikie.

Bwana, Mwumba na Mkombozi wa wanadamu wote, kwa unyenyekevu tunawaombea watu wote wa kila taifa walio katika dhiki yo yote ile:
- uwajulishe watu wa mataifa yote njia zako, na uwafunulie wokovu wako. (W.)

Kanisa lako liongozwe na kutawaliwa na Roho wako Mtakatifu;
- uwawezeshe wote wanaojiita Wakristo wafuate njia ya kweli, na washike imani yao kwa moyo mmoja. (W.)

Ee Baba, kwa wema wako uwasaidie wote wenye huzuni na mahangaiko;
- uwapatie kitulizo na upendo wa Roho wako Mtakatifu. (W.)

Baba, uwajalie marehemu wote uzima na pumziko:
- utujalie kushiriki pamoja nao utukufu wa Yesu Kristo, aliyekufa ili atuokoe. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Uwakumbuke watu wako, Ee Bwana, na uwaoneshe huruma yako: kama unavyowashibisha wenye njaa kwa chakula kitokacho mbinguni, ututajirishe sisi maskini kwa wingi wa neema zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.