Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 12 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

E Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Ee Bwana, nilikuita, nami nalitumainia neno lako.

Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.

Nakulilia, unisalimishe;*
nipate kuyashika mafundisho yako.

Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.

Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.

Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.

Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.

Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.

Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, nilikuita; nami nalitumainia neno lako.

ANT. II: Bwana ayajua mawazo ya wanadamu; ayajua kuwa ni batili.

Zab.94 Mungu hakimu wa wote
Bwana atawaadhibu wenye dhambi: maana Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali alituita tuishi katika utakatifu (1Tes.4:6-7)

I
Ee Mungu, Mungu mwenye kutoa adhabu,*
ewe Mungu mwenye kutoa adhabu, ujitokeze!

Usimame, ee hakimu wa watu wote;*
uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili!

Waovu wataona fahari hata lini?*
Watajisifia mpaka lini, Ee Mungu?

Hata lini waovu watajigamba kwa maneno?*
Watajivuna na kujitapa mpaka lini?

Wanawaangamiza watu wako, Ee Mungu,*
wanawakandamiza hao walio mali yako.

Wanawaua wajane na wageni;*
wanawachinja yatima!

Ati wanasema: “Mungu haoni;*
Mungu wa Yakobo hajui!”

Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo!*
Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa?

Aliyefanya sikio, je, yeye hawezi kusikia?*
Aliyeumba jicho, je, yeye hawezi kuona?

Mwenye kuyatawala mataifa, hawezi kuadhibu?/
Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa?*
Mungu ajua mawazo ya watu kuwa hayafai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ayajua mawazo ya wanadamu; ayajua kuwa ni batili.

ANT. III: Bwana amekuwa ngome yangu, na msaidizi mwenye nguvu ninayemtumainia.

II
Ee Mungu, heri mtu unayempa nidhamu,*
mtu unayemfundisha sheria yako.

Wakati wa taabu utampa kitulizo,*
hali waovu wanachimbiwa shimo.

Hakika Mungu hatawaacha watu wake;*
hatawasahau hao walio mali yake.

Basi, hukumu zitakuwa za haki tena,*
na waadilifu wote watazizingatia.

Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu?*
Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya?

Mungu asingalinisaidia,*
ningalikwisha enda kwenye nchi ya wafu.

Niliposema: “Naanguka,”*
upendo wako mkuu, Ee Mungu, ulinitegemeza.

Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi,*
wewe wanituliza na kunifurahisha.

Wewe huwezi kuhusiana na watawala dhalimu,*
wanaotunga sheria za kutetea maovu.

Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu,*
na kuwahukumu kifo watu wasio na hatia.

Lakini Mungu ni mlinzi wangu thabiti;*
Mungu wangu, ni mwamba wa usalama wangu.

Uovu wao atawarudishia wao wenyewe,/
atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao.*
Naam, Mungu, Mungu wetu, atawaangamiza!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana amekuwa ngome yangu, na msaidizi mwenye nguvu ninayemtumainia.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.10:24,31
Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake. Basi, cho chote mfanyacho, iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

K. Ni vema kumtukuza Bwana.
W. Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu.

SALA:
Tuombe: Mungu Mtakatifu na mwaminifu kwa ahadi zako, ulimtuma Roho wako kuwaunganisha watu waliotengana kwa sababu ya dhambi. Tujalie neema ili tuweze kuimarisha umoja na amani kati yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kol.3:17
Kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu, na kumshukuru Baba kwa njia yake.

K. Ee Bwana, nitakutolea sadaka ya sifa.
W. Nitaliita jina lako.

SALA:
Tuombe: Mungu mwenye uwezo na mapendo, ziangalie kwa huruma kazi tulizozianza; na utuongezee neema zako mchana huu; sahihisha kasoro zetu, ili kazi zetu ziweze kukamilika kadiri ya matakwa yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:23-24
Kila mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana, na si kwa ajili ya mtu. Kumbukeni kwamba Bwana atawapeni tuzo kile alichowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana!

K. Bwana ndiye urithi wangu.
W. Wewe ndiwe unijaliaye yote.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, ulinyoosha mikono yako msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; ujalie, kazi na maisha yetu yakupendeze, na yashuhudie uwezo na mapendo yako ya ukombozi. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.