JUMATANO JUMA 12 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 2Fal.22:8-13,23:1-3
Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya Bwana. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanyakazi wanaoisimamia nyumba ya Bwana. Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, akasema, Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa. Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya Bwana. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:33-37,40(K)33
1. Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako,
Nami nitaishika hata mwisho.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.

(K) Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.

2. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako,
Wala usiielekee tamaa. (K)

3. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,
Unihuishe katika njia yako.
Tazama, nimeyatamani mausia yako,
Unihuishe kwa haki yako. (K)

SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako kweli, ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!

INJILI: Mt.7:15-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuza matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.