Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tumwabudu Bwana, kwani ndiye aliyetuumba.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Bwana Mungu, wako mwanga
Utiao nyota kiza
Vitu vyote huamsha,
Na vyote vinavyopata
Katika Wewe uzima
Utukufuo huimba.

Uwepo wako mwanana,
Ambao nguvu hutoa,
Upo mahali po pote,
Na watu waloanguka
Waweze tena nyanyuka
Kwa hizo mbawa za sala.

Wewe ndiwe Mungu Mwema
Mwenye huruma kwa vyote,
Vyote ulivyoviumba;
Ulitupatia Kristo,
Ambaye kwa pendo lake
Akafa atukomboe.

Twakusifu Wewe Baba,
Pamoja na wako Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Ambaye katika Yeye
Vyote huishi, hudumu,
Na kupata pumziko.

ANT. I: Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Ee Bwana, maana nafsi yangu nakuinulia wewe.

Zab.86 Kuomba msaada
Atukuzwe Mungu... mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote (2Kor.1:3-4)

Unisikilize, Ee Mungu, unitegee sikio,*
maana mimi ni fukara na mnyonge.

Uilinde roho yangu, maana mimi ni mchaji wako;*
uniokoe mimi mtumishi wako, ninayekutegemea.

Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma.*
Mimi ninakulilia mchana kutwa.

Unifurahishe mimi mtumishi wako, Ee Mungu,*
maana sala zangu nazielekeza kwako.

Wewe, Ee Bwana, u mwema na mwenye huruma;*
umejaa upendo mkuu kwa wote wanaokuomba.

Usikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uangalie kilio cha ombi langu.

Siku za taabu nakuita,*
maana wewe wanisikiliza.

Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;*
hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.

Mataifa yote uliyoyaumba yatakuja na kukuabudu;*
yatatangaza ukuu wa jina lako.

Wewe ni mwenye enzi kuu, wafanya miujiza;*
wewe ndiwe Mungu peke yako.

Unifundishe, Ee Mungu, mwongozo wako,/
nami nitaufuata kwa uaminifu;*
uongoze moyo wangu nikuheshimu.

Nitakusifu, Ee Bwana, Mungu wangu, kwa moyo wote;*
nitatangaza ukuu wa jina lako hata milele.

Upendo wako ni mkuu mno!*
Umeniokoa kutoka chini kuzimu.

Ee Mungu, wenye kiburi wamenikabili;/
kundi la watu wakatili wanataka kuniua,*
watu ambao hawakujali wewe hata kidogo.

Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa huruma na mapendo;*
wewe ni mvumilivu, mpole na mwaminifu.

Unigeukie, unihurumie;/
unijalie nguvu yako, unisalimishe,*
mimi niliye mtumishi wako kama mama yangu.

Unioneshe ishara ya wema wako, Ee Mungu,/
ili wale wanaonichukia waaibike,*
wakiona wewe umenisaidia na kunifariji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Ee Bwana, maana nafsi yangu nakuinulia wewe.

ANT. II: Ana heri mtu anayetenda haki na kusema ukweli.

WIMBO: Isa.33:13-16 Mungu atatawala kwa haki
Ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali, na kwa ajili ya wowote wale ambao Bwana Mungu wetu atawaita kwake. (Mate.2:39)

Sikieni ninyi mlio mbali, niliyoyatenda;/.
na ninyi mlio karibu,*
kirini uweza wangu.

Wenye dhambi walio katika Sion wanaogopa;*
tetemeko limewashika wasiomcha Mungu;

Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao;*
ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

Ni yeye aendaye kwa haki,*
anenaye maneno ya adili;

ni yeye anayedharau faida*
ipatikanayo kwa dhuluma;

akung'utaye mikono yake*
asipokee rushwa;

azibaye masikio yake*
asisikie habari za damu;

afumbaye macho yake*
asitazame uovu.

Huyu ndiye atakayekaa juu;*
majabali ni ngome yake;

atapewa chakula chake;*
maji yake hayatakoma.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ana heri mtu anayetenda haki na kusema ukweli.

ANT. III: Mshangilieni Bwana, Mfalme.

Zab.98 Mungu mtawala dunia yote
Zaburi hii yaeleza ujio wa kwanza wa Bwana, na imani ya mataifa yote (Mt. Athanasius)

Mwimbieni Mungu, wimbo mpya,*
kwa maana ametenda mambo ya ajabu!

Kwa nguvu na enzi yake takatifu*
amejipatia ushindi.

Mungu ameonesha ushindi wake;*
ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa.

Ameshika ahadi aliyowapa watu wa Israeli,*
kwa upendo mkuu na uaminifu kwao.

Pande zote za dunia*
zimeuona ushindi wa Mungu wetu.

Dunia yote imshangilie Mungu;*
imsifu kwa nyimbo na vigelegele.

Msifuni Mungu kwa shangwe,*
kwa sauti za kinubi na zeze.

Mpigieni vigelegele Mungu mfalme wetu,*
mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.

Bahari ivume na vyote vilivyomo;*
dunia na wote waishio ndani yake.

Enyi mito, pigeni makofi;*
enyi vilima, imbeni pamoja kwa shangwe.

Shangilieni mbele ya Mungu,*
maana anakuja kutawala dunia.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,*
na watu atawatawala kwa uadilifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mshangilieni Bwana, Mfalme.

SOMO: Ayu.1:21;2:10b
Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vile vile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe. Je! tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?

KIITIKIZANO
K. Uelekeze moyo wangu kwenye utashi wako, Ee Mungu. (W. Warudie)
K. Unihuishe katika njia yako.
W. Ee Mungu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uelekeze...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Utuoneshe huruma yako, Ee Bwana; ulikumbuke agano lako takatifu.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina

Ant. Utuoneshe huruma yako, Ee Bwana; ulikumbuke agano lako takatifu.

MAOMBI
Mungu ni upendo: anayekaa katika pendo huishi ndani ya Mungu, na Mungu huwa ndani yake. Katika Yesu Kristo twaona jinsi Mungu anavyotupenda. Na tuiamshe imani yetu katika pendo lake Kristo.
W. Bwana Yesu umetupenda, ukajitoa sadaka kwa ajili yetu.

Umetujalia uzima na mwanga asubuhi hii:
- tunakushukuru kwa mapaji hayo. (W.)

Wewe ndiwe peke uliye Bwana wa wakati ujao:
- utujalie tusikate tamaa, na wala tusiogope mambo yajayo. (W.)

Upendo haujitafutii mambo yake:
- imarisha utashi wetu, ili tuachane na ubinafsi wetu leo. (W.)

Uwezeshe upendo wako ulio ndani yetu kushinda uovu wote:
- tuzidishie imani, matumaini na uvumilivu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, kwa hekima yako ulituumba, na kwa busara yako unatutawala: iangaze mioyo yetu kwa nuru yako takatifu, ili tukutumikie kiaminifu katika maisha yetu yote. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.