Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Kristo uwe karibu nami
Kulia na kushoto kwangu,
Kristo nyuma yangu simama,
Simama Kristo mbele yangu,
Kristo uwe pamoja nami
Po pote pale niendapo,
Kristo uwe kila upande,
Juu, chini na kandokando.

Kristo uwe moyoni mwangu
Na akilini mwangu pia,
Kristo uliye ndani yangu
Rohoni ulohifadhiwa,
Kristo tawala moyo wangu
Moyo mpotovu tiisha;
Kristo kamwe usiondoke,
Siondoke kwangu bakia.

Kristo ewe uzima wangu
Pekee ulo yangu njia,
Kristo uliye taa yangu
Kwa usiku na kwa mchana;
Kristo uwe rafiki yangu
Bila kugeukageuka,
Na uwe kiongozi wangu
Na mchungaji hata mwisho.

ANT. I: Waliopanda kwa machozi, watavuna kwa kelele za furaha.

Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu (2Kor.1:7)

Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!

Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.

Nao watu wa mataifa mengine walisema:*
“Mungu amewatendea mambo makubwa!“

Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!

Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu,/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.

Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe.

Wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Waliopanda kwa machozi, watavuna kwa kelele za furaha.

ANT. II: Bwana atatujengea nyumba; ataulinda mji wetu.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Ninyi ni jengo lake Mungu (1Kor.3:9)

Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana atatujengea nyumba; ataulinda mji wetu.

ANT. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote; yu juu ya yote.

WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbevyote, ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.

Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu

katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.

Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,

ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.

Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,

vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.

Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.

Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.

Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,

ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.

Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.

Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.

Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,

na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote; yu juu ya yote.

SOMO: Ef.3:20-21
Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu, aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.

KIITIKIZANO
K. Uniokoe, Ee Bwana, na unioneshe huruma yako. (W. Warudie)
K. Usiniangamize pamoja na wenye dhambi.
W. Unioneshe huruma yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uniokoe...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mwenyezi Mungu amenifanyia makuu, na jina lake ni takatifu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mwenyezi Mungu amenifanyia makuu, na jina lake ni takatifu.

MAOMBI
Naweza kuwa na imani kubwa ya kuweza hata kuhamisha milima: lakini kama sina upendo, mimi si kitu. Tukikumbuka hayo, tuombe:
W. Bwana, utujalie upendo wako.

Bwana, utuimarishe tunapojiunda na tunapokua kukuelekea wewe:
- utuongezee imani yetu wakati tunapofanya kazi. (W.)

Tumesongwa na wasiwasi, na kulemewa na mashaka,
- ifanye huru mioyo yetu, ili tuje kwako kwa matumaini. (W.)

Upendo hauhesabu maovu, wala haufurahii udhalimu:
- utusaidie tufurahie ukweli, na mapaji yako yanayoonekana katika wenzetu. (W.)

Uliimarishe Kanisa lako duniani katika imani ya mitume:
- utusaidie tuweze kupeana moyo tunaposhirikishana vipaji vyetu. (W.)

Uwajalie wale waliofariki dunia katika amani yako, ukamilifu wa imani yao na wa matumaini yao,
- uwape utimilifu wa upendo wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Kilio cha watu wako, Ee Bwana, kifike mbele yako. Uwasamehe dhambi zao, ili, kwa neema zako, waweze kujitoa kwa huduma zako, na wawe salama chini ya ulinzi wa mkono wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.