Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 15 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpуа.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;.
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Ye yote anifuataye, hatatembea gizani; bali atakuwa na mwanga wa uzima, asema Bwana.

Zab.119:105-112 XIV Sheria ya Mungu ni mwanga

Neno lako ni taa ya kuniongoza,*
na mwanga katika njia yangu.

Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,*
kwamba nitashika maagizo yako maadilifu.

Ee Mungu, ninateseka mno;*
unipe uhai kama ulivyoahidi.

Ee Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;*
na unifundishe maagizo yako.

Maisha yangu yamo hatarini daima,*
lakini siisahau sheria yako.

Waovu wamenitegea mitego kuninasa,*
lakini sikiuki amri zako.

Maagizo yako ni rasilmali yangu daima;*
naam, ni furaha ya moyo wangu.

Nimekusudia kwa moyo wote*
kutimiza kanuni zako milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ye yote anifuataye, hatatembea gizani; bali atakuwa na mwanga wa uzima, asema Bwana.

ANT. II: Mimi ni maskini na mhitaji; Ee Mungu, unisaidie.

Zab.70 Kuomba msaada
Bwana, utuokoe, tunaangamia (Mt.8:25)

Upende, Ee Mungu, upende kuniokoa;*
Ee Mungu, uje hima kunisaidia!

Waaibike na kufedheheka,*
hao wanaotaka kuniangamiza!

Warudishwe nyuma na kupata aibu,*
hao wanaofurahia maafa yangu!

Wapumbazike kwa aibu,*
hao wanaofurahia kunidhihaki!

Lakini wote wale wanaokutafuta,*
Wafurahi na kushangilia kwa sababu yako.

Wote wale wapendao nguvu yako ya kuokoa,*
waseme daima: “Mungu ni mkuu mno!"

Mimi niliye mnyonge na fukara,*
unijie hima, Ee Mungu!

Wewe ni msaada wangu, na mkombozi wangu;*
Ee Mungu, usikawie kunisaidia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mimi ni maskini na mhitaji; Ee Mungu, unisaidie.

ANT. III: Mungu hahukumu kufuata sura, bali hutawala kwa uadilifu na haki.

Zab.75 Mungu hakimu
Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao. vya enzi, akawakweza wanyenyekevu (Lk.1:52)

Tunakushukuru, Ee Mungu, tunakushukuru!/
Tunatangaza ukuu wako,*
na kusimulia juu ya matendo yako makuu.

"Mimi," asema Mungu, "nimeweka wakati maalum!*
Wakati huo nitatoa hukumu iliyo sawa.

Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo,*
mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake.

Nawaambia wenye kiburi: 'Acheni kujigamba!'*
na waovu: 'Msioteshe pembe za majivuno!

Msijione kuwa watu wa maana sana,*
hata kusema maneno ya kiburi.' "

Hukumu haiji kutoka mashariki au magharibi;*
wala haitoki nyikani au mlimani.

Mungu mwenyewe ndiye hakimu;*.
humshusha mmoja na kumkweza mwingine.

Mungu anashika kikombe mkononi,*
kimejaa divai kali ya hasira yake;

anaimimina, na waovu wote wanainywa;*
naam, wanainywa mpaka tone la mwisho.

Lakini mimi nitafurahi milele,*
nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo.

Atavunja nguvu zote za watu waovu;*
lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu hahukumu kufuata sura, bali hutawala kwa uadilifu na haki.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.13:4-7
Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauna wivu, haujidai, wala haujivuni. Upendo haukosi adabu, hautafuti faida yake binafsi, wala hauna wepesi wa hasira; hauweki kumbukumbu ya mabaya, haufurahii uovu, bali hufurahia ukweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.

K. Wafurahie na kushangilia, wote wakutafutao, Bwana.
W. Daima waseme: 'Mungu ni mkuu.'

SALA:
Tuombe: Mungu Mtakatifu na mwaminifu kwa ahadi zako, ulimtuma Roho wako kuwaunganisha watu waliotengana kwa sababu ya dhambi. Utujalie neema ili tuweze kuimarisha umoja na amani kati yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Kor.13:8-9,13
Upendo hauna kikomo. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita. Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili. Kwa sasa yapo mambo matatu: imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita hayo yote ni upendo.

K. Upendo wako uwe nasi, Ee Bwana.
W. Nasi twakutumainia kabisa wewe.

SALA:
Tuombe: Mungu mwenye uwezo na upendo, ziangalie kwa huruma kazi tulizozianza; na utuongezee neema zako mchana huu; sahihisha kasoro zetu, ili kazi zetu ziweze kukamilika kadiri ya matakwa yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:14-15
Zaidi ya yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!

K. Wanyenyekevu watairithi nchi.
W. Wataifurahia amani kamili.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, ulinyosha mikono yako msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; utujalie, kazi na maisha yetu vikupendeze na vishuhudie uwezo na mapendo yako ya ukombozi. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.