JUMATANO JUMA 18 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Yer.31:1-7
Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu. Bwana asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha. Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli, mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu. Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkasema, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli.

WIMBO WA KATIKATI: Yer.31:10-13(K)10
1. Lisikieni neno la Bwana,
Enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali,
Mkaseme Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake
Aliyekuwa hodari kuliko yeye.

(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

2. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni,
Wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai;
Na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe
Na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji;
Wala hawatauzunika tena kabisa. (K)

3. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja;
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji,
Na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)

SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!

INJILI: Mt.15:21-28
Yesu aliondoka Genezareti akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, Imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.