JUMATANO JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Yon.3:1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:1-2,10-11,16-17(K)17
1. Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.

(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu hutaudharau.

2. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho wako mtakatifu usiniondolee. (K)

3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. (K)

SHANGILIO: Eze.18:31
Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosea, Asema Bwana. Jifanyieni moyo mpya na roho mpya.

INJILI: Lk.11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

MAOMBI
Ndugu, sisi sote tunaalikwa kutubu dhambi zetu na kuwatangazia wenzetu habari hii ya toba. Ili neema ya Mungu ifanyekazi yake, tumwombe Yeye aliye Mpaji wa vyote.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Wahubiri wote wa Neno lako wawe tayari kwenda kokote wanakohitajika wanapotumwa kwa jina lako.

2. Utuwashie mapendo yako kwa wakosefu, ili tuwaendee na kuwahudumia bila ubaguzi.

3. Utuongezee imani, ili tusiwe watu wa kutaka ishara katika mambo yahusuyo hekima yako ya mbinguni.

4. Mwanao alifufuka siku ya tatu. Uwajalie marehemu wetu ufufuo na uzima usio na mwisho.

Ee Bwana Mungu, mahubiri ya Yona yaliwafanya watu wa Ninawi watubu na kuongoka. Uwajalie viongozi wote wa dini na serikali ushirikiano katika kukemea maovu, ili dunia ipate amani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.