Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'

Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.

Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.

ANT. I: Katika mwanga wako, Mungu, twaiona nuru.

Zab.36 Uovu wa binadamu
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima (Yoh.8:12)

Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake;*
wala jambo la kumcha Mungu, halimo kabisa kwake.

Kwa vile anajiona maarufu sana,/
anafikiri uovu wake hautagunduliwa*
na kulaaniwa na Mungu.

Kila asemacho ni uovu na uwongo*
ameacha kutumia hekima na kutenda mema.

Alalapo huwaza kutenda maovu,/
mwenendo wake hauna lolote jema,*
haepukani na chochote kibaya.

Wema wa Mungu
Ee Mungu, upendo wako mkuu/
wafika hata mbinguni;*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Uadilifu wako ni kama milima mikubwa mikubwa,/
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.*
Wewe, Ee Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama.

Upendo wako, Ee Mungu, ni mkuu ajabu:*
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.

Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;*
wawanywesha katika mto wa wema wako.

Wewe ndiwe asili ya uhai;*
kwa mwanga wako twaona mwanga.

wanaokutambua, uendelee kuwapenda;*
kwa waadilifu, uzidi kuwa mwema.

Usikubali wenye majivuno wanivamie,*
wala watu waovu wanikimbize.

Kumbe, watendao maovu wameanguka;*
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Katika mwanga wako, Mungu, twaiona nuru.

ANT. II: Ee Bwana, wewe u mkuu, wewe u mtukufu, wewe una nguvu ajabu.

WIMBO: Yud.16:1-2a,13-15 Bwana, mwumba wa dunia, huwalinda watu wake
Basi, wakaimba wimbo huu mpya (Ufu.5:9)

Mwimbieni Mungu wangu kwa matari;*
Mwimbieni Bwana wangu kwa matoazi;

Mwimbieni zaburi na nyimbo za shangwe;/
Mtukuzeni, mliitieni jina lake.*
Maana BWANA ndiye Mungu azivunjaye silaha za vita.

Nitamwimbia Mungu wangu wimbo mpya./
Ee BWANA, Wewe ndiwe mkuu, mwenye fahari;*
Wa ajabu katika uweza wako, hakuna kama Wewe.

Viumbe vyako vyote vikutumikie,*
Maana ulisema vikafanyika,

Ulitoa Roho vikaumbwa,*
Wala hakuna atakayeshindana na sauti yako.

Milima husukasuka katika misingi yake kama maji;/
Miamba huyeyuka kama nta mbele yako;*
Lakini u mwenye rehema kwao wanaokucha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, wewe u mkuu, wewe u mtukufu, wewe una nguvu ajabu.

ANT. III: Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.

Zab.47 Mtawala Mkuu
Ameketi kuume kwa Baba, na ufalme wake hautakuwa na mwisho

Enyi watu wote, pigeni makofi!*
Msifuni Mungu kwa shangwe!

Maana Mungu, Mungu Mkuu, anatisha.*
Ni mfalme mkuu wa ulimwengu wote.

Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa,*
ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.

Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu,*
ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.

Mungu amepanda juu huku akishangiliwa,*
Mungu amepanda juu akipigiwa tarumbeta.

Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni!*
Mwimbieni Mfalme wetu sifa, mwimbieni!

Mungu ni mfalme wa ulimwengu wote;*
mwimbieni sifa kwa tenzi.

Mungu anayatawala mataifa yote;*
amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu.

Watawala wa mataifa wanakusanyika,*
pamoja na watu wa Mungu wa Abrahamu.

Yeye ana nguvu kuliko majeshi yote,*
ametukuka juu yao wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.

SOMO: Isa.7:14b-15
Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema.

KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu wa Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Yu aja nyuma yangu aliye na nguvu zaidi kuliko mimi. Mimi sistahili kulegeza kamba za viatu vyake.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina

Ant. Yu aja nyuma yangu aliye na nguvu zaidi kuliko mimi. Mimi sistahili kulegeza kamba za viatu vyake.

MAOMBI
Neno wa Mungu amechagua kukaa kati yetu: kwa hiyo tumshukuru na kumtukuza.
W. Njoo, Bwana Yesu!

Uwatendee haki wale wanaolemewa na mateso:
- uwatetee maskini na wanyonge. (W.)

Mfalme wa Amani, utuondolee wivu na kututia upendo,
- utufundishe kuwasamehe wenzetu, badala ya kuwakasirikia. (W.)

Utakapokuja kuuhukumu ulimwengu,
- utuwezeshe kusimama mbele yako bila woga. (W.)

Upo kati yetu, lakini hujulikani:
- utusaidie tuweze kukuona katika maskini na wanaosumbuliwa. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, itayarishe mioyo yetu kwa nguvu ya neema yako. Kristo atakapokuja, atukute katika hali inayofaa kuupokea mkate wa mbingu katika karamu ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.