JUMATANO JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.
Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.
Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB
nuru yangu na wokovu wangu; nimwogope nani?
Zab.27 Kwa Mungu kuna usalama
Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu (Ufu.21:3)
I
Mungu ndiye mwanga wangu, na mwokozi wangu,*
nimwogope nani?
Mungu ni mlinzi wa maisha yangu;*
nitamwogopa nani basi?
Watu wabaya wakinivamia na kutaka kuniua,*
wao wenyewe watajikwaa na kuanguka.
Hata kama nikizungukwa na jeshi, sitaogopa;*
hata nikikabiliwa na vita, sitakufa moyo.
Jambo moja nimemwomba Mungu;*
jambo moja tu natafuta:
Nikae nyumbani mwa Mungu,*
siku zote za maisha yangu;
niuone uzuri wake Mungu,*
na kutafuta maongozi yake Hekaluni mwake.
Siku ya taabu atanihifadhi bandani mwake;/
atanificha katika hema yake,*
na kunisalimisha juu ya mwamba.
Nami nitawashinda adui zangu wanaonizunguka;/
nitatolea sadaka kwa shangwe Hekaluni mwake,*
nitaimba na kumshangilia Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu; nimwogope nani?
ANT. II: Ee Bwana, uso wako nautafuta; usinifiche uso wako.
Msaada wapatikana kwa Mungu
Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uwongo dhidi ya Yesu (Mk.14:57)
II
Usikie, Ee Mungu, ninapokulilia;*
unionee huruma na kunisikiliza.
Nafikiria uliyosema: “Njoo kwangu!"/
Naam, naja kwako; Ee Mungu.*
Usiache kuniangalia kwa wema.
Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;/
wewe umekuwa daima msaada wangu.*
Usinitupe wala usiniache, Ee Mungu mwokozi wangu.
Hata kama wazazi wangu wangenitupa,*
Mungu hatakosa kamwe kunitunza.
Ee Mungu, unifundishe njia yako;/
uniongoze katika njia iliyo sawa,*
kwa sababu adui zangu ni wengi.
Usiniache adui wanitende wapendavyo;*
mashahidi wa uwongo wanikabili kwa vitisho.
Naamini nitauona wema wake Mungu,*
katika makao ya walio hai.
Jiaminishe kwake Mungu!/
Piga moyo konde, usikate tamaa!*
Jiaminishe kwake Mungu!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Ee Bwana, uso wako nautafuta; usinifiche uso wako.
ANT. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza katika viumbe vyote, ni mkuu
juu ya viumbe vyote.
WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbevyote,
ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.
Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu
katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.
Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,
ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.
Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,
vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.
Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.
Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.
Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,
ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.
Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.
Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.
Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,
na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza katika viumbe vyote, ni mkuu
juu ya viumbe vyote.
SOMO: 1Kor.4:5
Basi, msihukumu kabla ya wakati wake, acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo
ya giza yaliyofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa
anayostahili kutoka kwa Mungu.
KIITIKIZANO
K. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe. (W. Warudie)
K. Utuoneshe uso wa tabasamu, nasi tutakuwa salama.
W. Njoo kwetu, utuokoe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana, Mungu...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Sheria itatangazwa kutoka Sion, na neno la Bwana litasikika kutoka Yerusalemu.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Sheria itatangazwa kutoka Sion, na neno la Bwana litasikika
kutoka Yerusalemu.
MAOMBI
Tumwombe Mungu Baba, aliye Bwana na Mtawala wa wote.
W. Uwajie watu wako!
Njoo, ewe mchungaji, uliangalie kundi lako;
- uwakusanye watu wote katika Kanisa moja. (W.)
Bwana, uwakumbuke wana wote wa Abrahamu,
- wote wanaoingojea ahadi yako kwa imani. (W.)
Tunawaombea wote wanaokata tamaa ya kuishi;
- Bwana, uwape tumaini litakalowasaidia kuishi, na ujasiri wa kuvumilia mateso.
(W.)
Uwakumbuke wale waliofariki dunia;
- uwaoneshe utukufu, ambao Mwanao aliupata kwa ajili yao. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana
yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana, itayarishe mioyo yetu kwa nguvu ya neema yako. Kristo atakapokuja, atukute katika
hali inayofaa kuupokea mkate wa mbinguni katika karamu ya milele. Tunaomba hayo kwa njia
ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu,
daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.