Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 1 MAJILIO
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

Zab.119:9-16 II Uaminifu kwa Sheria ya Mungu
Kijana atatunzaje mwenendo wake uwe safi?*
Kwa kuyashika maagizo yako.

Najitahidi kukutii kwa moyo wote;*
unijalie kuzishika amri zako.

Nimeshika agizo lako moyoni mwangu,*
nisije nikakukosea.

Utukuzwe, Ee Mungu!*
Unifundishe kanuni zako.

Nitazirudia kwa sauti*
sheria zako zote ulizotoa.

Nafurahi kufuata amri zako,*
kuliko kuwa na utajiri mwingi.

Nazitafakari amri zako,*
na kuyazingatia maagizo yako.

Nazifurahia kanuni zako;*
sitazisahau amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.17 Sala ya mtu mwema
Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye akasikilizwa (Ebr.5:7)

I
Ee Mungu, unisikilize niombapo haki zangu;/
usikilize kilio changu,*
upokee ombi langu la moyo mnyofu.

Utatoa hukumu ya kunifadhili,*
kwani wewe wajua jambo la haki.

Wewe waujua kabisa moyo wangu;/
umenijia usiku, umenichunguza;*
hukuona uovu wowote ndani yangu.

Sisemi maovu, kama wafanyavyo wengine;*
nimeitii amri yako, sikuishika njia ya wadhalimu.

Nimefuata daima njia yako;*
wala sikuiacha kamwe.

Nakuita, Ee Mungu, kwani wanisikiliza;*
unitegee sikio, uyasikilize maneno yangu.

Onyesha upendo wako mkuu,/
uwaokoe kutoka kwa adui zao,*
wale wanaokukimbilia.

Unilinde kama mboni ya jicho lako;/
unifiche kivulini mwa mabawa yako,*
mbali na mashambulio ya waovu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Adui wa hatari wanizunguka,/
hawana huruma yoyote ile;*
wamejaa maneno ya kujigamba.

Sasa wamenizingira pande zote;*
wanavizia waniangushe chini.

Wako tayari kunirarua kama simba;*
kama aviziavyo mawindo mwana-simba.

Uje, Ee Mungu, kuwakabili na kuwaporomosha.*
Kwa upanga wako uniokoe na watu waovu;

kwa mkono wako, Ee Mungu, uniokoe na watu hao,*
watu ambao huthamini riziki ya dunia hii tu.

Waadhibu kwa mateso uliyowawekea,/
yawe ya kutosha kwa watoto wao,*
wawaachie na wajukuu wao.

Lakini mimi nitakuona, kwani sikutenda ubaya;*
niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Isa.2:11
Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Isa.12:2
Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; nitatumaini wala sitaogopa, maana BWANA YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu. Naye amekuwa wokovu wangu.

K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo, utuokoe.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Dan.9:19
Ee BWANA, usikie; Ee BWANA, usamehe; Ee BWANA usikilize; ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.

K. Njoo, Ee Bwana usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka dhambi zao.

SALA:
Tuombe: Bwana, itayarishe mioyo yetu kwa nguvu ya neema yako. Kristo atakapokuja, atukute katika hali inayofaa kuupokea mkate wa mbingu katika karamu ya milele. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.