JUMATANO JUMA LA 33
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tumwabudu Bwana, kwani ndiye aliyetuumba.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Bwana Mungu, wako mwanga
Utiao nyota kiza
Vitu vyote huamsha,
Na vyote vinavyopata
Katika Wewe uzima
Utukufuo huimba.
Uwepo wako mwanana,
Ambao nguvu hutoa,
Upo mahali po pote,
Na watu waloanguka
Waweze tena nyanyuka
Kwa hizo mbawa za sala.
Wewe ndiwe Mungu Mwema
Mwenye huruma kwa vyote,
Vyote ulivyoviumba;
Ulitupatia Kristo,
Ambaye kwa pendo lake
Akafa atukomboe.
Twakusifu Wewe Baba,
Pamoja na wako Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Ambaye katika Yeye
Vyote huishi, hudumu,
Na kupata pumziko.
ANT. I: Katika mwanga wako, Mungu, twaiona nuru.
Zab.36 Uovu wa binadamu
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima (Yoh.8:12)
Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake;*
wala jambo la kumcha Mungu, halimo kabisa kwake.
Kwa vile anajiona maarufu sana,/
anafikiri uovu wake hautagunduliwa*
na kulaaniwa na Mungu.
Kila asemacho ni uovu na uwongo*
ameacha kutumia hekima na kutenda mema.
Alalapo huwaza kutenda maovu,/
mwenendo wake hauna lolote jema,*
haepukani na chochote kibaya.
Wema wa Mungu
Ee Mungu, upendo wako mkuu/
wafika hata mbinguni;*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.
Uadilifu wako ni kama milima mikubwa mikubwa,/
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.*
Wewe, Ee Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama.
Upendo wako, Ee Mungu, ni mkuu ajabu:*
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;*
wawanywesha katika mto wa wema wako.
Wewe ndiwe asili ya uhai;*
kwa mwanga wako twaona mwanga.
wanaokutambua, uendelee kuwapenda;*
kwa waadilifu, uzidi kuwa mwema.
Usikubali wenye majivuno wanivamie,*
wala watu waovu wanikimbize.
Kumbe, watendao maovu wameanguka;*
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Katika mwanga wako, Mungu, twaiona nuru.
ANT. II: Ee Bwana, wewe u mkuu, wewe u mtukufu, wewe una nguvu ajabu.
WIMBO: Yud.16:1-2a,13-15 Bwana, mwumba wa dunia, huwalinda watu wake
Basi, wakaimba wimbo huu mpya (Ufu.5:9)
Mwimbieni Mungu wangu kwa matari;*
Mwimbieni Bwana wangu kwa matoazi;
Mwimbieni zaburi na nyimbo za shangwe;/
Mtukuzeni, mliitieni jina lake.*
Maana BWANA ndiye Mungu azivunjaye silaha za vita.
Nitamwimbia Mungu wangu wimbo mpya./
Ee BWANA, Wewe ndiwe mkuu, mwenye fahari;*
Wa ajabu katika uweza wako, hakuna kama Wewe.
Viumbe vyako vyote vikutumikie,*
Maana ulisema vikafanyika,
Ulitoa Roho vikaumbwa,*
Wala hakuna atakayeshindana na sauti yako.
Milima husukasuka katika misingi yake kama maji;/
Miamba huyeyuka kama nta mbele yako;*
Lakini u mwenye rehema kwao wanaokucha.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Ee Bwana, wewe u mkuu, wewe u mtukufu, wewe una nguvu ajabu.
ANT. III: Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.
Zab.47 Mtawala Mkuu
Ameketi kuume kwa Baba, na ufalme wake hautakuwa na mwisho
Enyi watu wote, pigeni makofi!*
Msifuni Mungu kwa shangwe!
Maana Mungu, Mungu Mkuu, anatisha.*
Ni mfalme mkuu wa ulimwengu wote.
Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa,*
ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.
Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu,*
ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.
Mungu amepanda juu huku akishangiliwa,*
Mungu amepanda juu akipigiwa tarumbeta.
Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni!*
Mwimbieni Mfalme wetu sifa, mwimbieni!
Mungu ni mfalme wa ulimwengu wote;*
mwimbieni sifa kwa tenzi.
Mungu anayatawala mataifa yote;*
amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu.
Watawala wa mataifa wanakusanyika,*
pamoja na watu wa Mungu wa Abrahamu.
Yeye ana nguvu kuliko majeshi yote,*
ametukuka juu yao wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.
SOMO: Tob.4:16-17,19
Wenye njaa uwape baadhi ya chakula chako, na walio uchi uwape baadhi ya nguo zako;
sawasawa na wingi wako utoe sadaka; wala utoapo sadaka jicho lako lisiwe na choyo.
Utoe chakula kwa ukarimu kwenye maziko ya wenye haki; lakini waovu usiwape kitu.
Umhimidi BWANA, `Mungu wako, siku zote. Umwombe Yeye ili njia zako zinyoshwe,
na mapito yako yote na mashauri yako yote yafanikiwe.
KIITIKIZANO
K. Uelekeze moyo wangu kwenye utashi wako, Ee Mungu. (W. Warudie)
K. Unihuishe katika njia yako.
W. Ee Mungu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uelekeze...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Utuoneshe huruma yako, Ee Bwana; ulikumbuke agano lako takatifu.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina
Ant. Utuoneshe huruma yako, Ee Bwana; ulikumbuke agano lako
takatifu.
MAOMBI
Tunamshukuru na kumsifu Kristo, kwa sababu hakuona haya kutuita sisi ndugu zake. Kwa hiyo
tumwombe:
W. Ututakatifuze nduguzo, Ee Bwana.
Utusaidie tuweze kuishi maisha mapya ya Pasaka,
- ili kwa njia yetu watu watambue nguvu ya upendo wako. (W.)
Kila siku ni alama ya mapendo yako kwetu;
- ututie mapendo yako, leo, katika mioyo yetu. (W.)
Utuwezeshe kukuona katika watu wote;
- utusaidie tuweze kukutambua wewe hasa katika wale wanaoteseka. (W.)
Maisha yetu leo yajae huruma yako;
- utujalie hali ya kusamehe, na moyo wa ukarimu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Ee Mungu Mwokozi wetu, kwa neema ya ubatizo umetufanya watoto wa nuru. Isikie sala yetu,
ili tuweze kuishi katika nuru hiyo daima, na kuushuhudia ukweli wako mbele ya watu.
Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na
Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.