Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 33
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Kristo uwe karibu nami
Kulia na kushoto kwangu,
Kristo nyuma yangu simama,
Simama Kristo mbele yangu,
Kristo uwe pamoja nami
Po pote pale niendapo,
Kristo uwe kila upande,
Juu, chini na kandokando.

Kristo uwe moyoni mwangu
Na akilini mwangu pia,
Kristo uliye ndani yangu
Rohoni ulohifadhiwa,
Kristo tawala moyo wangu
Moyo mpotovu tiisha;
Kristo kamwe usiondoke,
Siondoke kwangu bakia.

Kristo ewe uzima wangu
Pekee ulo yangu njia,
Kristo uliye taa yangu
Kwa usiku na kwa mchana;
Kristo uwe rafiki yangu
Bila kugeukageuka,
Na uwe kiongozi wangu
Na mchungaji hata mwisho.

ANT. I: Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu; nimwogope nani?

Zab.27 Kwa Mungu kuna usalama
Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu (Ufu.21:3)

I
Mungu ndiye mwanga wangu, na mwokozi wangu,*
nimwogope nani?

Mungu ni mlinzi wa maisha yangu;*
nitamwogopa nani basi?

Watu wabaya wakinivamia na kutaka kuniua,*
wao wenyewe watajikwaa na kuanguka.

Hata kama nikizungukwa na jeshi, sitaogopa;*
hata nikikabiliwa na vita, sitakufa moyo.

Jambo moja nimemwomba Mungu;*
jambo moja tu natafuta:

Nikae nyumbani mwa Mungu,*
siku zote za maisha yangu;

niuone uzuri wake Mungu,*
na kutafuta maongozi yake Hekaluni mwake.

Siku ya taabu atanihifadhi bandani mwake;/
atanificha katika hema yake,*
na kunisalimisha juu ya mwamba.

Nami nitawashinda adui zangu wanaonizunguka;/
nitatolea sadaka kwa shangwe Hekaluni mwake,*
nitaimba na kumshangilia Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu; nimwogope nani?

ANT. II: Ee Bwana, uso wako nautafuta; usinifiche uso wako.

Msaada wapatikana kwa Mungu
Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uwongo dhidi ya Yesu (Mk.14:57)

II
Usikie, Ee Mungu, ninapokulilia;*
unionee huruma na kunisikiliza.

Nafikiria uliyosema: “Njoo kwangu!"/
Naam, naja kwako; Ee Mungu.*
Usiache kuniangalia kwa wema.

Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;/
wewe umekuwa daima msaada wangu.*
Usinitupe wala usiniache, Ee Mungu mwokozi wangu.

Hata kama wazazi wangu wangenitupa,*
Mungu hatakosa kamwe kunitunza.

Ee Mungu, unifundishe njia yako;/
uniongoze katika njia iliyo sawa,*
kwa sababu adui zangu ni wengi.

Usiniache adui wanitende wapendavyo;*
mashahidi wa uwongo wanikabili kwa vitisho.

Naamini nitauona wema wake Mungu,*
katika makao ya walio hai.

Jiaminishe kwake Mungu!/
Piga moyo konde, usikate tamaa!*
Jiaminishe kwake Mungu!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, uso wako nautafuta; usinifiche uso wako.

ANT. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza katika viumbe vyote, ni mkuu juu ya viumbe vyote.

WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbevyote, ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.

Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu

katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.

Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,

ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.

Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,

vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.

Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.

Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.

Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,

ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.

Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.

Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.

Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,

na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Yeye ni mzaliwa wa kwanza katika viumbe vyote, ni mkuu juu ya viumbe vyote.

SOMO: Yak.1:22,25
Msijidanganye wenyewe, kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.

KIITIKIZANO
K. Uniokoe, Ee Bwana, na unionyeshe huruma yako. (W. Warudie)
K. Usiniangamize pamoja na wenye dhambi.
W. Unionyeshe huruma yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uniokoe...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

MAOMBI
Dunia inang'aa kwa utukufu wa Mungu, ambaye huwatunza watu wake wateule kwa mapendo yasiyo na mwisho. Kwa jina la Kanisa, na tusali:
W. Bwana, onesha mapendo yako kwa watu wote.

Ulikumbuke Kanisa lako:
- uliepushe na maovu yote, na ulikamilishe katika mapendo yako. (W.)

Uwawezeshe watu wote kutambua kuwa wewe peke yako ndiwe Mungu, na kwamba Yesu Kristo ni Mwana wako;
- uwape mwanga wa imani. (W.)

Utujalie tuweze kuwafikiria wale ambao kazi zao ni ngumu na hazina pato:
- na utuwezeshe kumpa kila mtu heshima anayostahili. (W.)

Uwape amani wote waliofariki dunia leo;
- uwajalie pumziko la milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Usikilize, Ee Bwana, sala yetu, na utulinde mchana na usiku, ili sisi tunaohangaishwa na mabadiliko ya wakati, tupate kuwa imara katika wewe, mwamba wetu usiye badilika. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.