JUMATANO JUMA LA 33
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
ANT. I: Umehimidiwa, Ee Bwana; unifundishe amri zako.
Zab.119:9-16 II Uaminifu kwa Sheria ya Mungu
Kijana atatunzaje mwenendo wake uwe safi?*
Kwa kuyashika maagizo yako.
Najitahidi kukutii kwa moyo wote;*
unijalie kuzishika amri zako.
Nimeshika agizo lako moyoni mwangu,*
nisije nikakukosea.
Utukuzwe, Ee Mungu!*
Unifundishe kanuni zako.
Nitazirudia kwa sauti*
sheria zako zote ulizotoa.
Nafurahi kufuata amri zako,*
kuliko kuwa na utajiri mwingi.
Nazitafakari amri zako,*
na kuyazingatia maagizo yako.
Nazifurahia kanuni zako;*
sitazisahau amri zako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Umehimidiwa, Ee Bwana; unifundishe amri zako.
ANT. II: Ziimarishe hatua zangu katika njia zako, Ee Bwana.
Zab.17 Sala ya mtu mwema
Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba
Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye akasikilizwa (Ebr.5:7)
I
Ee Mungu, unisikilize niombapo haki zangu;/
usikilize kilio changu,*
upokee ombi langu la moyo mnyofu.
Utatoa hukumu ya kunifadhili,*
kwani wewe wajua jambo la haki.
Wewe waujua kabisa moyo wangu;/
umenijia usiku, umenichunguza;*
hukuona uovu wowote ndani yangu.
Sisemi maovu, kama wafanyavyo wengine;*
nimeitii amri yako, sikuishika njia ya wadhalimu.
Nimefuata daima njia yako;*
wala sikuiacha kamwe.
Nakuita, Ee Mungu, kwani wanisikiliza;*
unitegee sikio, uyasikilize maneno yangu.
Onyesha upendo wako mkuu,/
uwaokoe kutoka kwa adui zao,*
wale wanaokukimbilia.
Unilinde kama mboni ya jicho lako;/
unifiche kivulini mwa mabawa yako,*
mbali na mashambulio ya waovu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Ziimarishe hatua zangu katika njia zako, Ee Bwana.
ANT. III: Inuka, Ee Bwana, uiokoe roho yangu.
II
Adui wa hatari wanizunguka,/
hawana huruma yoyote ile;*
wamejaa maneno ya kujigamba.
Sasa wamenizingira pande zote;*
wanavizia waniangushe chini.
Wako tayari kunirarua kama simba;*
kama aviziavyo mawindo mwana-simba.
Uje, Ee Mungu, kuwakabili na kuwaporomosha.*
Kwa upanga wako uniokoe na watu waovu;
kwa mkono wako, Ee Mungu, uniokoe na watu hao,*
watu ambao huthamini riziki ya dunia hii tu.
Waadhibu kwa mateso uliyowawekea,/
yawe ya kutosha kwa watoto wao,*
wawaachie na wajukuu wao.
Lakini mimi nitakuona, kwani sikutenda ubaya;*
niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Inuka, Ee Bwana, uiokoe roho yangu.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 1Pet.1:13-14
Muwe tayari kabisa kwa nia, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika baraka ile
mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! Kama watoto wa Mungu wenye utii,
msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga.
K. Bwana, unijulishe njia zako.
W. Unifundishe mapito yako.
SALA:
Tuombe: Mungu Mtakatifu na mwaminifu kwa ahadi zako, ulimtuma Roho wako kuwaunganisha watu
waliotengana kwa sababu ya dhambi. Utujalie neema ili tuweze kuimarisha umoja na amani
kati yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Pet.1:15-16
Mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni
mtakatifu. Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu."
K. Makasisi wako watavishwa utakatifu.
W. Waamini wako watafanya shangwe.
SALA:
Tuombe: Mungu mwenye uwezo na upendo, ziangalie kwa huruma kazi tulizozianza; na utuongezee neema
zako mchana huu: sahihisha kasoro zetu, ili kazi zetu ziweze kukamilika kadiri ya matakwa
yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Yak. 4:7-8a,10
Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Shetani, naye atawakimbieni. Mkaribieni Mungu,
naye atakuja karibu nanyi. Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.
K. Bwana huwaangalia wale wanaomheshimu.
W. Yupo karibu na wale wanaotumainia upendo wake.
SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, ulinyosha mikono yako msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu;
utujalie, kazi na maisha yetu vikupendeze na vishuhudie uwezo na mapendo yako ya
ukombozi. Unayeishina kutawala daima na milele.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.