Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 34
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe Utatu, Nuru tukufu,
Ewe Umoja, Wa enzi kuu,
Jua 'mezama, Basi chomoza
Yako mionzi, Mwetu nyoyoni.

Twakutolea, Wimbo wa sifa
Asubuhi, na, Jioni sala;
Pamwe maombi, Twasifu sana
Yako adhama, Milele yote.

ANT. I: Tunangojea kwa matumaini, baraka za ujio mtukufu wa Mwokozi wetu.

Zab.62 Mungu mlinzi wangu
Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu (Rom.15:13)

Kimya kimya namngojea tu Mungu;*
kwake watoka wokovu wangu.

Yeye peke yake ndiye mwamba wa wokovu wangu,*
yeye ni ngome yangu, sitashindwa.

Hata lini mtamshambulia mtu/
aliye kama kiambaza kilichoinama,*
kama ukuta unaoanza kubomoka?

Naam, toka mahali pake pa heshima,*
mnakusudia tu kumwangusha.

Furaha yenu ni kusema uwongo./
Kwa maneno mnabariki,*
lakini moyoni mnalaani.

Kimya kimya namgojea tu Mungu;*
kwake naliweka tumaini langu.

Yeye peke yake ndiye mwamba wa wokovu wangu,*
yeye ni ngome yangu, sitashindwa.

Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu;*
Mungu ni mwamba wa usalama na kimbilio langu.

Enyi watu, mtumainieni Mungu daima;*
mwelezeni shida zenu; Mungu ni kimbilio letu.

Binadamu wote ni kama pumzi tu;*
wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu.

Tena, ukiwapima uzito hawafikii kilo,*
wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi.

Msitegemee ujambazi,/
msijisifie mali ya wizi;*
kama mali zikiongezeka msizitegemee.

Mungu ametamka mara moja,/
nami nimesikia tena na tena:*
kwamba enzi ni mali yake Mungu;

wewe, Ee Bwana, ndiwe mwenye upendo mkuu.*
Wewe wamlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Tunangojea kwa matumaini, baraka za ujio mtukufu wa Mwokozi wetu.

ANT. II: Mungu na atubariki; na atuangaze kwa nuru ya uso wake.

Zab.67 Wimbo wa shukrani
Jueni, basi, kwamba wokovu utokao kwa Mungu umepelekwa kwa watu wa mataifa (Mate.28:28)

Utuonee huruma, Ee Mungu, utubariki;*
utuelekezee uso wako kwa wema;

dunia yote itambue mwongozo wako,*
mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Mataifa yote yafurahi na kushangilia;/
maana wawahukumu watu kwa haki,*
na kuyaongoza mataifa ya dunia.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Nchi imetoa mazao yake;*
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.

Mungu ametujalia baraka zake,*
watu wote duniani wamche.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mungu na atubariki; na atuangaze kwa nuru ya uso wake.

ANT. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.

Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu

katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.

Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,

ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.

Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,

vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.

Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.

Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.

Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,

ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.

Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.

Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.

Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,

na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

SOMO: 1Pet.5:5b-7
Ninyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu, mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu." Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni.

KIITIKIZANO
K. Utulinde, Ee Bwana, kama mboni ya jicho lako. (W. Warudie)
K. Utufiche kivulini mwa mabawa yako.
W. Ee Bwana, utulinde.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utulinde...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ee Bwana, onesha nguvu za mkono wako; uwashushe wenye kiburi, uwapandishe wanyenyekevu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ee Bwana, onesha nguvu za mkono wako; uwashushe wenye kiburi, uwapandishe wanyenyekevu.

MAOMBI
Jioni hii tumshukuru Mungu Baba ambaye, kwa njia ya Kristo, alifanya upatanisho baina yake na ulimwengu mzima.
W. Utukufu kwako, Ee Bwana Mungu!

Tunakushukuru kwa uzuri wa ulimwengu:
- kazi za binadamu zisiuharibu uzuri huo, bali ziukuze ili kuonesha zaidi utukufu wako. (W.)

Baba, tunakushukuru kwa mema yote tunayopata:
- utufunze kuyapokea kwa shukrani, na kuyatumia ipasavyo. (W.)

Utufundishe kutafuta mambo yale yakupendezayo,
- ndipo tutakapoweza kukuona wewe katika yote tutendayo. (W.)

Bwana, tunaposafiri kuelekea kwenye nchi ya ahadi, utulishe kwa mkate wa mbinguni,
- zima kiu yetu kwa maji ya uzima. (W.)

Kwako, miaka elfu ni kama siku moja:
- wachukue wale waliokufa wakiwa na tumaini kwako, na uwaingize katika uzima wa milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Mungu Mwenyezi, jina lako ni takatifu, na huruma yako hudumu kizazi hata kizazi: pokea sala ya watu wako, na uwajalie waweze kuutukuza ukuu wako milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.