Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 34
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Nimezitafakari njia zangu, na nimeyarudia mapenzi yako.

Zab.119:57-64 VIII Heshima kwa sheria ya Mungu
Ee Mungu, ndiwe uliye pekee muhimu kwangu;*
naahidi kushika maagizo yako.

Nakusihi kwa moyo wangu wote;*
unionee huruma kama ulivyoahidi!

Nimeufikiria mwenendo wangu,*
na ninaahidi kuyafuata maagizo yako.

Bila kukawia nafanya haraka*
kuzishika amri zako.

Ingawa mitego ya wakosefu inanisonga,*
lakini sisahau sheria yako.

Usiku wa manane naamka kukusifu,*
kwa sababu ya hukumu zako adilifu.

Mimi ni rafiki ya wote wakuchao,*
wa wote wanaozitii amri zako.

Dunia imejaa upendo wako mkuu, Ee Mungu;*
unifundishe kanuni zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nimezitafakari njia zangu, na nimeyarudia mapenzi yako.

ANT. II: Hofu na tetemeko limenijia; unielekee na kusikiliza kilio changu, Ee Bwana.

Zab.55:1-14,16-23 Sala ya mtu anayedhulumiwa
Yesu akaanza kufadhaika sana na kuhangaika (Mt.14:33)

I
Ee Mungu, sikiliza sala yangu;*
usilipe kisogo ombi langu.

Unisikilize na kunikubalia;*
nimechoshwa na mahangaiko yangu.

Nina hofu kubwa kwa vitisho vya adui zangu,*
na kwa kudhulumiwa na watu waovu.

Watu waovu wananitaabisha,*
na kwa hasira wananifanyia uhasama.

Moyo wangu umejaa hofu,*
vitisho vya kifo vimenisonga.

Natetemeka kwa hofu kubwa,*
nimevamiwa na vitisho vikubwa.

Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa!*
Ningeruka mbali na kupata pumziko;

naam, ningesafiri mbali sana,*
na kupata makao jangwani.

Ningekimbilia mahali pa usalama,*
mbali na upepo mkali na dhoruba.

Ee Bwana, vuruga lugha yao;*
maana naona ukatili na ugomvi mjini,

vikiuzunguka usiku na mchana,*
na kuujaza maafa na jinai.

Uharibifu umeenea pote mjini,*
uhasama na ukandamizaji kila mahali.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Hofu na tetemeko limenijia; unielekee nakusikiliza kilio changu, Ee Bwana.

ANT. III: Nitamlilia Mungu, naye Bwana ataniokoa.

II
Kama adui yangu angenitukana,*
ningeweza kustahimili hayo;

kama mpinzani wangu angenidharau,*
ningeweza kujificha mbali naye.

Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu;*
ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!

Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki;*
pamoja tulifanya ibada nyumbani mwa Mungu.

Lakini mimi namlilia Mungu,*
naye Mungu ataniokoa.

Jioni, asubuhi na adhuhuri,/
nalalama na kulia kwa huzuni,*
naye ataisikia sauti yangu.

Ataniokoa na kunisalimisha*
katika vita ninavyovikabili, dhidi ya maadui wengi.

Mungu atawalaye tangu milele,/
atatega sikio na kuwashinda;*
maana hawashiki sheria wala kumcha Mungu.

Mwenzangu amewashambulia rafiki zake,*
amevunja mapatano yake.

Maneno yake laini kuliko siagi,*
lakini moyo wake watamani vita.

Maneno yake mororo kama mafuta,*
lakini yanakata kama upanga mkali.

Mwachie Mungu mzigo wako,/
naye atakutegemeza;*
kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.

Lakini wauaji na wabaya,*
Mungu atawaporomosha shimoni mwa maangamizi,

kabla ya kufikia nusu ya maisha yao.*
Lakini mimi nitakutumainia wewe, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Nitamlilia Mungu, naye Bwana ataniokoa.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Kum.1:16-17a
Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye. Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu.

K. Bwana ni mwenye haki, hupenda njia za haki.
W. Waadilifu watauona uso wake.

SALA:
Tuombe: Mungu Mtakatifu na mwaminifu kwa ahadi zako, ulimtuma Roho wako kuwaunganisha watu waliotengana kwa sababu ya dhambi. Utujalie neema ili tuweze kuimarisha umoja na amani kati yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Isa.55:8-9
Mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kwa vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

K. Bwana Mungu Mwenyezi, nani yu sawa nawe?
W. Unao uwezo, Ee Bwana, na ukweli ni vazi lako.

SALA:
Tuombe: Mungu mwenye uwezo na upendo, uziangalie kwa huruma kazi tulizozianza; na utuongezee neema zako mchana huu: sahihisha kasoro zetu, ili kazi zetu ziweze kukamilika kadiri ya matakwa yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Sam.16:7b
BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.

K. Unichunguze, Ee Mungu, na uujue moyo wangu.
W. Uniongoze katika njia ya uzima wa milele.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, ulinyosha mikono yako msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; utujalie kazi na maisha yetu vikupendeze, na vishuhudie uwezo na mapendo yako ya ukombozi. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.