JUMATANO YA MAJIVU
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Hek.11:24,25,26
Ee Bwana, wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba. Unawasamehe watu dhambi zao ili wapate kutubu, na kuwahurumia, kwa kuwa ndiwe Bwana Mungu wetu.

KOLEKTA:
Ee Bwana, utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya kiroho kwa mfungo mtakatifu, ili katika kushindana na jeshi la pepo wabaya, tulindwe na misaada ya kujinyima. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Yoe.2:12-18
Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia Baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, na hao wanyonyao maziwa; bwana arusi na atoke chumbani mwake, na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie kati ya patakatifu na madhabahu, na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, wala usiutoe urithi wako upate aibu, hata mataifa watawale juu yao; kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao? Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:1-4,10-12,15
1. Ee Mungu, nirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.

(K) Uturehemu, Ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi.

2. Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)

3. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

4. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

SOMO 2: 2Kor.5:20–6:2
Ndugu zangu, basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.

SHANGILIO: Zab.95:8
Msifanye migumu mioyo yenu; msikie sauti ya Bwana.

INJILI: Mt.6:1-6, 16-18
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampatai thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amini, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amini, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

MAOMBI
Ndugu zangu, leo tunapoalikwa kutubu, tumwombe Bwana Mungu wetu ambaye si mwepesi wa hasira atujalie neema zake.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Makuhani na wahudumu wote wa Bwana wasichoke kutupelekea mbele yako sala na maombi yetu ya msamaha wa dhambi.

2. Uwajalie waamini wote kutambua kuwa siku ya wokovu ndiyo sasa, ili waweze kuzitumia vema neema wanazozipata kwako.

3. Utuepushe sisi sote na kishawishi cha kufanya wema kwa kujionesha mbele za watu; na uwalipe mara dufu wale wanaotufadhili kwa mapendo ya kweli.

4. Uwapokee katika ufalme wako ndugu zetu marehemu, hasa wale waliojitahidi kutimiza masharti ya mfungo na mapendo kwa jirani.

Ee Baba yetu mwema, uzidi kutuneemesha ili juhudi zetu za kusali, kufunga, kupokea masakramenti na kutenda matendo ya huruma katika mfungo huu tunaouanza zituletee wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, kwa kutoa dhabihu hii ya kuanzia rasmi Kwaresima, tunakuomba kuzishinda tamaa mbaya kwa njia ya matendo ya kitubio na upendo. Nasi tukiisha takaswa dhambi, tustahili kuwa na moyo wa ibada wa kuadhimisha mateso yake Mwanao. Anayeishi na kutawala milele na milele.

ANTIFONA YA KOMUNYO:
Mwenye kuitafakari sheria ya Bwana mchana na usiku, atazaa matunda yake kwa majira yake.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti tuliyoipokea itupatie msaada, ili kufunga kwetu kukupendeze, na kutufae kwa kutuponya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Mungu, tunakuomba umimine kwa wema roho ya toba juu ya hawa waamini walioinama mbele ya adhama yako, na kwa huruma yako wastahili kuzifikia thawabu zilizoahidiwa kwa wale wanaofanya toba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.