Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tuje mbele ya Bwana kwa shukrani

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Siku hujaa wangavu
Mungu aletapo mwanga
Kutoka nuru angavu,
Na ndipo viumbe vyote
Vilivyofanyika upya
Hufurahi mbele yake.

Yeye Baba huonesha
Ajabu za ulimwengu
Kwa sisi watoto wake,
Ajabu zionyeshazo,
Kama bendera angani,
Nguvuze na utukufu.

Asubuhi na mapema
Sisi na kila kiumbe
Ambacho kina uhai
Mungu tunamwelekea,
Ambaye ni Baba yetu,
Na kumuomba kwa moyo:

Ewe Baba, Ewe Mwana,
Nawe Roho, tunaomba
Neema na msamaha,
Ili tuishi vizuri
Tukusifu wewe Mungu
Leo na mpaka mwisho.

ANT. I: Wewe ndiwe nikuombaye, Ee Bwana; asubuhi wanisikia.

Zab.5:1-9,11-13 Sala wakati wa hatari
Wale waliopokea Neno la Mungu ambalo lakaa ndani yao, watafurahi milele.

Ee Mungu, uyasikie maneno yangu;*
uyasikilize malalamiko yangu.

Usikilize kilio changu,/
Ee Mungu, mfalme wangu;*
maana wewe ndiwe nikuombaye.

Ee Mungu, alfajiri waisikia sauti yangu,/
asubuhi nakutolea sadaka yangu,*
kisha nakutazamia.

Wewe si Mungu wa kupenda uovu;*
kwako hawezi kukaa mtu mwovu.

Wenye majivuno hawastahimili mbele yako;*
wewe wawachukia wote watendao maovu.

Wawaangamiza wote wasemao uwongo;*
wawachukia wauaji na wadanganyifu.

Lakini, kwa upendo wako mkuu,*
mimi nitaingia nyumbani mwako;

nitaabudu kwa uchaji,*
katika Hekalu lako takatifu.

Kwa uadilifu wako, Ee Mungu, uniongoze,/
kwa sababu adui zangu ni wengi;*
uiweke njia yako wazi mbele yangu.

Maneno ya adui zangu hayaaminiki,*
nia yao ni kuleta maangamizi;

wanabubujika maneno ya kubembeleza,*
lakini kwa kweli ni maneno ya kuua.

Lakini wote wakukimbiliao wafurahi;*
daima waimbe kwa shangwe.

Uwalinde wanaolipenda jina lako;*
ili wafurahi kwa sababu yako.

Maana wewe Mungu, wambariki mwadilifu;*
kama ngao, wamkinga kwa fadhili yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Wewe ndiwe nikuombaye, Ee Bwana; asubuhi wanisikia.

ANT. II: Ee Bwana, Mungu wetu, twalisifu jina lako tukufu.

WIMBO: 1Nya.39:10-13 Heshima na utukufu viwe kwa Mungu peke yake
Atukuzwe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu kristo (Ef.1:3)

Uhimidiwe, Ee BWANA,/
Mungu wa Israeli baba yetu,*
milele na milele.

Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza,*
na utukufu, na kushinda, na enzi;

maana vitu vyote*
vilivyo mbinguni na duniani ni vyako.

Ufalme ni wako, Ee BWANA,/
nawe umetukuzwa,*
u mkuu juu ya vitu vyote.

Utajiri na heshima hutoka kwako wewe,*
nawe watawala juu ya vyote;

na mkononi mwako mna uweza na nguvu;*
tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.

Basi sasa, Mungu wetu,*
twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, Mungu wetu, twalisifu jina lako tukufu.

ANT. III: Mwabuduni Mungu katika makao yake matakatifu.

Zab.29 Sauti ya Mungu katika dhoruba
Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye" (Mt.3:17)

Msifuni Mungu, enyi viumbe vya mbinguni;*
msifuni Mungu mtukufu na mwenye nguvu.

Lisifuni jina tukufu la Mungu;*
mwabuduni Mungu anapotokea.

Sauti ya Mungu yasikika juu ya maji mengi;/
Mungu mtukufu ananguruma,*
sauti ya Mungu yasikika juu ya bahari!

Sauti ya Mungu ina nguvu,*
sauti ya Mungu imejaa fahari.

Sauti ya Mungu huvunja mierezi;*
naam, hata mierezi ya Lebanoni.

Huifanya milima ya Lebanoni/
irukeruke kama ndama,*
na mlima Hermoni kama mwana-nyati.

Sauti ya Mungu hutoa miali ya moto./
Sauti ya Mungu hutetemesha jangwa;*
Mungu atetemesha jangwa la kadeshi.

Sauti ya Mungu huitikisa mivule;*
hukwanyua majani ya miti msituni,

wakazi Hekaluni mwake wote wasema:*
"Utukufu kwa Mungu!"

Mungu atawala juu ya gharika:*
Mungu ni mfalme, atawala milele.

Mungu atawapa watu wake nguvu:*
atawabariki watu wake na amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mwabuduni Mungu katika makao yake matakatifu.

SOMO: 2Tes.3:10b-13
'Mtu ye yote anayekataa kufanya kazi, hana ruhusa ya kula chakula.' Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu, na ambao hawafanyi cho chote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi, ili wajipatie masilahi yao wenyewe. Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema.

KIITIKIZANO
K. Atukuzwe Bwana, karne hata karne. (W. Warudie)
K. Yeye pekee ametenda maajabu.
W. karne hata karne.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Atukuzwe...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Atukuzwe Bwana, Mungu wetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Atukuzwe Bwana, Mungu wetu.

MAOMBI
Siku mpya inapoanza, tumsifu Kristo ambaye ndani yake mna Roho wa Mungu, na utimilifu wa neema.
W. Utujalie Roho wako, Ee Bwana.

Twakusifu wewe Bwana,
- na tunakushukuru kwa baraka zako. (W.)

Utujalie utulivu na moyo wa ukarimu;
- utujalie afya na nguvu, ili tuweze kutimiza matakwa yako (W.)

Upendo wako udumu nasi leo;
- utuongoze katika kazi zetu. (W.)

Uwe nao wote wanaohitaji sala zetu,
- na uwajalie mahitaji yao yote. (W.)


Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, uwe mwanzo na mwisho wa yote tunayofanya na tunayosema. Kwa neema yako utusaidie katika matendo yetu, na uyakamilishe hayo kwa uwezo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.