Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njooni msifuni Bwana,
Msifuni Baba Mwenyezi,
Mfalme wa mataifa yote!
Itangazeni sifa yake,
Enyi watu kwa makelele!
Pendo lake yakini kweli;
Neno lake laaminika,
Neno lake kweli thabiti,
Kwa vizazi vyote milele!

Sifa kwake Baba, Rahimu,
Bwana wa wote ulimwengu!
Sifa kwa Mwanae twatoa,
Mwokozi alotukomboa!
Ewe Hua, Njiwa wa mbingu,
Sifa kwako zije kwa wingi
Mtoa wa faraja zote,
Ewe tunda la Pendo lao,
Pendo la Baba na la Mwana. Amina.

ANT. I: Bwana anawatunza wanyonge na wanaoonewa.

Zab.11 Mtumaini Mungu
Mungu ndiye kimbilio langu!/
Mbona mwaniambia:*
"Ruka kama ndege, kimbilia mlimani?

Tazama waovu wanavyovuta upinde;/
wameweka mishale tayari juu ya uta,*
wawapige mshale gizani watu wema.

Kama misingi ikiharibiwa,*
mtu mwadilifu atafanya nini?"

Mungu yumo katika Hekalu lake takatifu;*
kiti cha enzi cha Mungu kiko mbinguni.

Macho yake huwaangalia wanadamu,*
na anajua wanachofanya.

Mungu huwapima waadilifu na waovu;*
huwachukia kabisa watu wakatili.

Atawanyeshea wakosefu makaa ya moto;*
kiberiti na upepo wa hari vitakuwa adhabu yao.

Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu;*
wanyofu watamwona.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana anawatunza wanyonge na wanaoonewa.

ANT. II: Heri wenye moyo safi: maana watamwona Mungu.

Zab.15 Rafiki ya Mungu
Ee Mungu, nani awezaye kukaa hemani mwako?*
nani awezaye kukaa juu ya mlima wako mtakatifu?

Ni mtu anayeishi bila hatia,/
atendaye daima yaliyo sawa,*
asemaye ukweli kutoka moyoni,

na ambaye hasengenyi watu./
Ni mtu ambaye hamtendei ubaya mwenzake,*
wala hamfitini jirani yake.

Mtu huyo huwadharau wafisadi,/
lakini huwaheshimu wamchao Mungu.*
Hutimiza ahadi yake hata kama ikimtia hasara.

Hukopesha bila kutaka faida,/
wala hali rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.*
Mtu mwenye sifa hizo, atakuwa imara milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Heri wenye moyo safi: maana watamwona Mungu.

ANT. III: Mungu alituchagua katika Mwanae, akatufanya tuwe wanawe.

WIMBO: Ef.1:3-10 Azimio la Mungu kuhusu wokovu
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu alituchagua katika Mwanae, akatufanyatuwe wanawe.

SOMO: Kol.1:9b-11
Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana, na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema, na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu, ili mweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.

KIITIKIZANO
K. Uniponye roho yangu, maana nimekukosea. (W. Warudie)
K. Nikasema: 'Unihurumie, Ee Bwana.'
W. Maana nimekukosea.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uniponye...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Moyo wangu wamtukuza Bwana, kwa kuwa ameutazama unyonge wangu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Moyo wangu wamtukuza Bwana, kwa kuwa ameutazama unyonge wangu.

MAOMBI
Mungu Baba yetu, amefanya nasi agano la milele. Kwa shukrani na imani tumwombe:
W. Bwana, uwabariki watu wako.

Uwaokoe watu wako, Ee Bwana,
- na ulibariki taifa lako. (W.)

Uwaunganishe Wakristo wote katika kundi moja,
- ili dunia ipate kumwamini Kristo uliyemtuma kwetu. (W.)

Bwana, uwabariki watu wako. Uwajalie neema rafiki zetu na wajuani wetu wote,
- na ueneze mapendo ya Kristo kati yao. (W.)

Uwatulize walio mahututi;
- uwajalie watambue mapendo ya wokovu wako.( (W.)

Uwahurumie marehemu;
- wapate pumziko katika Kristo. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Kwa ibada yetu hii utukuzwe, Ee Mungu, Wewe, ambaye kwa ajili ya wokovu wetu, uliutazama unyenyekevu wa Maria, mtumishi wako. Utuwezeshe kushiriki naye ukamilifu wa ukombozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.