Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 13 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT. I: Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo, na kuyatia macho mwanga.

Zab.19B:7-14. Sheria ya Mungu
Basi, mwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu (Mt.5:48)

Sheria ya Mungu ni kamilifu,*
humrudishia mtu nguvu;

agizo la Mungu ni thabiti,*
huwapa hekima wasio na makuu.

Amri za Mungu ni sawa,*
hufurahisha moyo;

agizo la Mungu ni la haki,*
humwelimisha mtu.

Kumcha Mungu ni jambo jema,*
uchaji wa Mungu wadumu milele;

hukumu za Mungu ni sawa,*
zote nizahaki kabisa.

Zatamanika kuliko dhahabu;*
kulikodhahabu safi kabisa.

Ni tamu kuliko asali;*
kuliko asali safi kabisa.

Zanifunza mimi mtumishi wako;*
kuzitii kwaniletea tuzo kubwa.

Lakini nani ayaonaye makosa yake mwenyewe?*
Ee Mungu, niepushe na makosa yale nisiyoyajua.

Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi,*
usikubali hayo yanitawale.

Hapo nitakuwa mkamilifu;*
sitakuwa na dhambi kubwa.

Maneno na mawazo yangu yakupendeze, Ee Mungu,*
mwamba wa usalama wangu na mkombozi wangu!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo, na kuyatia macho mwanga.

ANT. II: Bwana atakuja kuyahukumu mataifa kwa haki.

Zab.7 Sala ya mtu anayedhulumiwa
Hakimu yu karibu, tayari kuingia (Yak.5:9)

I
Ee Mwenyezi, Mungu wangu, nakukimbilia wewe;*
uniokoe na wote wanaonidhulumu, unisalimishe.

La sivyo, watakuja kama simba kunirarua,/
na mbali kunivutia,*
pasiwe na mtu wa kuniokoa.

Ee Mwenyezi, Mungu wangu!/
Kama nimetenda moja ya mambo haya:*
kama nimechafua mikono yangu kwa ubaya,

kama nimemtenda vibaya rafiki yangu,*
au nimemshambulia bila sababu adui yangu,

basi, adui na anifuatie na kunikamata;/
ayakanyage maisha yangu;*
nakuniulia mbali.

Ee Mungu, uje kwa ghadhabu yako;*
uikabili hasira ya adui zangu.

Inuka, Ee Mwenyezi,*
Wewe wataka daima haki itekelezwe.

Uyakusanye mataifa kando kando yako,*
nawe uwatawale kutoka juu.

Wewe, Ee Mungu, wayahukumu mataifa;/
unihukumu kwa kadiri ya uadilifu wangu,*
kadiri ya huo unyofu wangu.

Uukomeshe uovu wa watu wabaya,*
umwimarishe mtu mwema;

Ee Mungu utendaye haki,*
upimaye mioyo na akili.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana atakuja kuyahukumu mataifa kwa haki.

ANT. III: Jinsi Mungu alivyo mwamuzi mwenye haki na mwenye nguvu! Huwaokoa wanyofu wa moyo.

II
Mungu ni ngao yangu inayonilinda;*
yeye awaokoa watu wanyofu.

Mungu ni hakimu wa haki;*
kila siku humwadhibu adui mwovu.

Watu wasipoongoka, Mungu atanoa upanga wake;*
atavuta upinde wake na kulenga shabaha.

Atatayarisha silaha zake za hatari,*
na kuipasha moto mishale yake.

Lakini waovu wamejaa udhalimu;*
wameshiba uovu na watazaa udanganyifu.

Wamewachimbia wengine mashimo,*
lakini wao wenyewe watatumbukia humo.

Ubaya wao utawarudia wao wenyewe;*
ukatili wao utawaangukia wao wenyewe.

Nami nitamsifu Mungu kwa sababu ya wema wake;*
nitaimba sifa zake Mungu, Mungu Mkuu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Jinsi Mungu alivyo mwamuzi mwenye haki na mwenye nguvu! Huwaokoa wanyofu wa moyo.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Rom.13:8,10
Msiwe na deni kwa mtu ye yote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye binadamu mwenzake ameitekeleza Sheria. Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, kwa mapendo Sheria yote hutimizwa.

K. Umekuwa msaada wangu, usinitupe;
W. Wala usiniache, Ee Mungu, msaada wangu.

SALA:
Tuombe: Ee Baba Mwema, Mwumba wa vyote, umewaamuru watu wote kufanya kazi katika ulimwengu wako, na kwa ushirikiano wao, kuinua hali ya binadamu. Utujalie daima tuweze kufanya kazi pamoja kama watoto wa familia yako, na kuwapenda watu wote kidugu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Yak.1:19-20,26
Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, lakini si mwepesi wa kusema, na si mwepesi wa kukasirika. Maana hasira ya mtu haiwezi kuleta uadilifu wa Mungu. Kama mtu akijiona ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.

K. Nitamtukuza Bwana kila wakati.
W. Midomo yangu itasimulia sifa zake daima.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu, Bwana na Mkuu wa ulimwengu wote, unayetupangia kazi na kutupatia mastahili ya kazi zetu. Tunakuomba utusaidie tuweze kuvumilia taabu zote za leo, na kutekeleza kwa furaha matakwa yako katika yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Pet.1:17-18a,19
Mnapomtaja Mungu ninyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu, bila ubaguzi, kila mmoja kadiri ya matendo yake. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu. Maana mnajua kwamba ninyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa, ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu, si kwa vitu vyenye kuharibika, bali mlikombolewa kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye alikuwa kama Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.

K. Uniokoe, Ee Bwana, na unioneshe huruma yako.
W. Nitamtukuza Bwana katika hadhara ya watu.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu, unatualika tusali muda huu ambapo mitume walikwenda hekaluni kusali. Tunakuomba kwa moyo mnyofu, uwajalie wokovu wote wanaokuomba kwa jina la Yesu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.