Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 14 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe Nguvu na Tegemeo
La viumbe vyote po pote,
Unadumu milele yote
Bila hata kutingisika;
Lakini kwa utaratibu
Waongoza mabadiliko
Yote ya mwanga kila siku,
Na saa baada ya saa.

Kipe kitambo cha maisha
Mwisho mtulivu kabisa,
Jioni isiyofunikwa
Na vivuli vinavyonuka,
Utujalie tufe vema,
Tufe kitakatifu sana,
Ili tuvikwe utukufu
Wa asubuhi ya milele.

Utusikie, Ewe Baba,
Mhisani, mwenye huruma,
Kwa njia ya Yesu Kristo,
Neno wako hata milele,
Ambaye, pamoja na Roho,
Roho wako Mtakatifu,
Anaabudiwa milele
Na kila kilo na uhai.

ANT. I: U mzuri wa kupendeza kuliko wanadamu wote; neema imemiminwa midomoni mwako.

Zab.45 Utenzi wa arusi ya kifalme
Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki (Mt.25:6)

I
Moyo wangu umejaa mawazo mema:/
namtungia mfalme shairi langu,*
ulimi wangu u tayari kama kalamu ya mwandishi mwepesi:

wewe u mzuri kuliko wanadamu wote,/
maneno yako ni fadhili tupu,*
naye Mungu amekubariki milele.

Ewe shujaa, weka upanga wako tayari;*
wewe ni mtukufu na mwenye fahari.

Songa mbele kwa ushindi, utetee haki na ukweli,*
mkono wako ukupatie ushindi mkubwa.

Mishale yako ni mikali,/
hupenya mioyo ya adui za mfalme;*
nayo mataifa huanguka chini yako.

Utawala wako ni kama wa Mungu, wadumu milele;*
wewe wawatawala watu wako kwa haki.

Wapenda uadilifu na kuchukia uovu./
Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua,*
na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako.

Mavazi yako yanukia marashi na udi,/
wanamuziki wakuimbia katika majumba*
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu.

Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki,/
naye malkia amesimama kulia kwako,*
amevaa mapambo ya dhahabu safi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: U mzuri wa kupendeza kuliko wanadamu wote; neema imemiminwa midomoni mwako.

ANT. II: Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.

II
Nawe binti sikiliza! Nisikilize kwa makini:*
sahau sasa watu wako na jamaa zako.

Uzuri wako wamvutia mfalme;*
yeye ni bwana wako, lazima umtii.

Watu wa Turo watakuletea zawadi;*
matajiri watataka upendeleo wako.

Binti mfalme anaingia - mzuri kabisa!*
Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.

Amevalia vazi la rangi nyingi,*
aongozwa kwa mfalme

akisindikizwa na wanawali wenzake,*
nao pia wanapelekwa kwa mfalme.

Kwa furaha na shangwe wanafika huko,*
na kuingia katika jumba la mfalme.

Ee mfalme, utapata watoto wengi/
watakaotawala badala ya wazee wako;*
utawafanya watawale duniani kote.

Sifa zako, nitazieneza kwa vizazi vyote daima,*
nayo mataifa yatakusifu daima na milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.

ANT. III: Mungu alikusudia kuvijumlisha vitu vyote katika Kristo, utimilifu wa wakati utakapowadia.

WIMBO: Ef.1:3-10 Mungu Mwokozi
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu alikusudia kuvijumlisha vitu vyote katika Kristo, utimilifu wa wakati utakapowadia.

SOMO: 1Tes.2:13
Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: Tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

KIITIKIZANO
K. Ee Bwana, sala yangu ifike mbele yako. (W. Warudie)
K. Ipande kwako kama moshi wa ubani.
W. Ifike mbele yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ee Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ee Mungu wangu, moyo wangu na utangaze ukuu wako milele.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ee Mungu wangu, moyo wangu na utangaze ukuu wako milele.

MAOMBI
Tutoe shukrani kwa Kristo, Bwana wetu, ambaye hulipenda na kulitunza Kanisa lake.
W. Uwe karibu nasi, Ee Bwana, jioni hii.

Bwana Yesu, uwajalie watu wote waweze kuokoka,
- na waujue ukweli. (W.)

Umlinde Papa F..., na Askofu wetu F...:
- Bwana Mwenyezi, uwasaidie kwa huruma yako. (W.)

Uwatie nguvu wale walio katika shida na huzuni;
- amsha tena ndani yao imani na hali ya kutambua maongozi ya Mungu. (W.)

Kristo, Bwana wetu mpendwa, kwa wema wako uwe na wagonjwa na maskini, wanyonge na wanaokufa:
- uwapatie kitulizo chako. (W.)

Uwapokee wale wote ambao, katika maisha yao, walishiriki ukuhani wako;
- uwajalie wakusifu milele mbinguni. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Mungu Mwenyezi, uliyetujalia, sisi watumishi wako tusiostahili, nguvu ya kufanyia kazi siku ya leo, twakuomba upokee sadaka yetu ya jioni hii, ambayo ni shukrani yetu kwa neema ulizotujalia. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.