JUMATATU JUMA 17 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Yer.13:1-11
Bwana aliniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la Bwana, nikajivika viunoni. Nalo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche karibu na mto Frati, kama Bwana alivyoniamuru. Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa, tena kwa lolote. Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, Bwana asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ile kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lolote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli, na nyumba yote ya Yuda, asema Bwana; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.

WIMBO WA KATIKATI: Kumb.32:18-21(K)18
1. Hukumbuki Mwamba aliyekuzaa,
Mungu aliyekuzaa umemsahau.
Bwana akaona, akawachukia,
Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.

(K) Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.

2. Akasema, nitawaficha uso wangu,
Nitaona mwisho wao utakuwaje;
Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,
Watoto wasio imani ndani yao. (K)

3. Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu,
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu.
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. (K)

SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!

INJILI: Yn.11:19-27
Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Maratha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.