Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 19 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tuje mbele ya Bwana kwa shukrani

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Siku hujaa wangavu
Mungu aletapo mwanga
Kutoka nuru angavu,
Na ndipo viumbe vyote
Vilivyofanyika upya
Hufurahi mbele yake.

Yeye Baba huonesha
Ajabu za ulimwengu
Kwa sisi watoto wake,
Ajabu zioneshazo,
Kama bendera angani,
Nguvuze na utukufu.

Asubuhi na mapema
Sisi na kila kiumbe
Ambacho kina uhai
Mungu tunamwelekea,
Ambaye ni Baba yetu,
Na kumuomba kwa moyo:

Ewe Baba, Ewe Mwana,
Nawe Roho, tunaomba
Neema na msamaha,
Ili tuishi vizuri
Tukusifu wewe Mungu
Leo na mpaka mwisho.

ANT. I: Wana heri wakaao nyumbani mwako, Bwana.

Zab.84 Hamu ya kuwapo nyumbani mwa Mungu
Hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja (Ebr.13:14)

Napenda mno makao yako,*
Ee Mungu mwenye nguvu!

Natamani kuwa Hekaluni mwa Mungu./
Kwa moyo na mwili wangu wote,*
namshangilia Mungu aliye hai.

Hata shomoro wamepata makao kwako;/
mbayuwayu wamejenga viota kwako,*
na kuweka makinda yao madhabahuni pako.

Ewe Mungu mwenye nguvu,*
Mfalme wangu na Mungu wangu!

Wana heri wakaao nyumbani mwako,*
ambamo waweza kukusifu daima.

Wana heri wanaopata nguvu kwako,*
wanaotamani kwenda kuhiji Mlima Sion.

Wapitapo katika bonde kavu,/
hulifanya kuwa chemchemi,*
na mvua za kwanza hulijaza madimbwi.

Wanaendelea kupata nguvu waendapo;*
watamwona Mungu wa miungu katika Sion.

Ee Mungu mwenye nguvu, sikia sala yangu.*
Unisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.

Umwangalie kwa wema, Ee Mungu wetu,*
umwangalie mfalme uliyemteua.

Siku moja Hekaluni mwako,*
ni bora kuliko siku elfu mahali pengine;

hata kusimama mlangoni pa nyumba yako,*
kuliko kukaa kwa watu waovu.

Mungu ni mlinzi wetu na mfalme mtukufu;*
hutuneemesha na kutujalia fahari.

Mungu hawanyimi chochote chema,*
wale ambao wanaishi bila hatia.

Ee Mungu mwenye nguvu,*
heri wale wanaokutumainia wewe!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Wana heri wakaao nyumbani mwako, Bwana.

ANT. II: Njooni, twende juu mlimani kwa Bwana.

WIMBO: Isa.2:2-5 Mlima wa nyumba ya Bwana utainuliwa juu ya vilima
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu (Ufu.15:4)

Na itakuwa katika siku za mwisho,/
mlima wa nyumba ya BWANA*
utawekwa imara juu ya milima,

nao utainuliwa juu ya vilima;/
na mataifa yote*
watauendea makundi makundi:

Na mataifa mengi watakwenda na kusema,/
Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA,*
nyumbani kwa Mungu wa Yakobo,

naye atatufundisha njia zake,*
nasi tutakwenda katika mapito yake;

maana katika Sion itatoka sheria,*
na neno la BWANA katika Yerusalemu.

Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi,*
atawakemea watu wa kabila nyingi;

nao watafua panga zao ziwe majembe,*
na mikuki yao iwe miundu;

taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine,*
wala hawatajifunza vita tena kamwe.

Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni,*
twende katika nuru ya BWANA.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Njooni, twende juu mlimani kwa Bwana.

ANT. III: Mwimbieni Bwana, litukuzeni jina lake.

Zab.96 Mungu mfalme na hakimu
Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi, na mbele ya Mwana-Kondoo (Ufu.14:3)

Mwimbieni Mungu, wimbo mpya!*
Mwimbieni Mungu, ulimwengu wote!

Mwimbieni Mungu na kulisifu jina lake./
Tangazeni kila siku habari njema*
kwamba ametuokoa.

Yatangazieni mataifa utukufu wake,*
na matendo yake makuu kwa watu wote.

Maana Mungu ni mkuu, anasifika sana;*
astahili kuheshimiwa zaidi kuliko miungu yote.

Miungu ya mataifa mengine si kitu;*
lakini Mungu aliziumba mbingu.

Utukufu na fahari vyamzunguka;*
enzi na uzuri vyalijaza Hekalu lake.

Mpeni Mungu heshima, enyi jamii zote za watu;*
sifuni utukufu na enzi yake.

Lisifuni jina tukufu la Mungu;*
leteni sadaka na kuingia Hekaluni mwake.

Mwabuduni Mungu anapotokea,*
tetemeka mbele yake, ee dunia nzima.

Yaambieni mataifa: “Mwenyezi ni mfalme!/
Ameufanya ulimwengu imara, hautatikisika.*
Atawahukumu watu kwa haki."

Furahini, enyi mbingu na dunia!*
Bahari na zivume pamoja na vyote vilivyomo!

Furahini, enyi mashamba na vyote vilivyomo!*
Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha,

Mungu atakapotokea kutawala dunia.*
Naam, atawatawala watu kwa haki na usawa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mwimbieni Bwana, litukuzeni jina lake.

SOMO: Yak.2:12-13
Semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. Maana, Mungu hatakuwa na huruma kwa mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.

KIITIKIZANO
K. Atukuzwe Bwana, karne hata karne. (W. Warudie)
K. Yeye pekee ametenda maajabu.
W. karne hata karne.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Atukuzwe...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Atukuzwe Bwana, Mungu wetu.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Atukuzwe Bwana, Mungu wetu.

MAOMBI
Mungu ametuonesha heshima ya kufanya kazi, kwa maisha ya Mwanae aliyejifanya mtu; tuombe:
W. Bwana, uzibariki kazi zetu.

Tunakutukuza, Bwana, kwa kutuwezesha kuamka salama;
- tunakushukuru kwa kutulinda na kutujalia mahitaji yetu. (W.)

Uwe nasi, Bwana, tunapofanya kazi zetu za kila siku;
- na utujalie tukumbuke kwamba tunakaa na kufanya kazi katika ulimwengu wako. (W.)

Umetuita tukutumikie ipasavyo katika ulimwengu huu;
- utusaidie kujenga jumuiya ya haki na ya Kikristo. (W.)

Ukae nasi, na uwe na kila mmoja tutakayekutana naye leo;
- utujalie tuweze kueneza furaha na amani yako duniani. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, Mfalme wa mbingu na dunia, tawala mioyo na miili yetu leo. Ututakase na uyaongoze mawazo, maneno na matendo yetu yafuate amri zako, ili sasa na siku zote, neema yako ituokoe na kutufanya huru. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.