Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 19 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njooni msifuni Bwana,
Msifuni Baba Mwenyezi,
Mfalme wa mataifa yote!
Itangazeni sifa yake,
Enyi watu kwa makelele!
Pendo lake yakini kweli;
Neno lake laaminika,
Neno lake kweli thabiti,
Kwa vizazi vyote milele!

Sifa kwake Baba, Rahimu,
Bwana wa wote ulimwengu!
Sifa kwa Mwanae twatoa,
Mwokozi alotukomboa!
Ewe Hua, Njiwa wa mbingu,
Sifa kwako zije kwa wingi
Mtoa wa faraja zote,
Ewe tunda la Pendo lao,
Pendo la Baba na la Mwana. Amina.

ANT. I: Macho yetu yamwelekea Bwana; tunatazamia huruma yake.

Zab.123 Kuomba huruma.
Vipofu wawili...walipaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuonee huruma!" (Mt.20:30)

Ninakuinulia macho yangu, Ee Mungu*
unayekaa huko juu mbinguni.

Kama watumishi wamtegemeavyo bwana wao,*
kama mjakazi amtegemeavyo bibi yake,

ndivyo tunavyokutegemea wewe, Ee Mungu, Mungu wetu,*
mpaka hapo utakapotuonea huruma.

Utuhurumie, Ee Mungu, utuhurumie,*
maana tumedharauliwa mno.

Tumedharauliwa na wadhalimu wenye kiburi,*
tumepuuzwa vya kutosha na matajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Macho yetu yamwelekea Bwana; tunatazamia huruma yake.

ANT. II: Msaada wetu watoka kwa jina la Bwana, aliyeumba mbingu na dunia.

Zab.11 Mungu kinga yetu
Bwana alimwambia Paulo katika ono: "Usiogope,... maana mimi nipo pamoja nawe" (Mate.18:9-10)

Haya Israeli, sasa useme:*
"Kama Mungu asingalikuwa upande wetu,

kweli Mungu asingalikuwa upande wetu,*
wakati ule tuliposhambuliwa na watu,

hakika tungalimezwa wazima-wazima,*
wakati hasira zao zilipotuwakia.

Hapo tungalikumbwa na gharika,/
tungalifunikwa na mto wa maji,*
mkondo wa maji ungalituchukua.“

Atukuzwe Mungu,*
asiyetuacha makuchani mwao.

Tumeponyoka kama ndege*
katika mtego wa wawindaji!

Mtego umeteguliwa,*
nasi tukaokoka.

Msaada wetu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Msaada wetu watoka kwa jina la Bwana,aliyeumba mbingu na dunia.

ANT. III: Mungu ametuchagua, akatufanya tuwe watoto wake katika Mwana wake.

WIMBO: Ef.1:3-10 Azimio la Mungu kuhusu wokovu
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu ametuchagua, akatufanya tuwe watoto wake katika Mwana wake.

SOMO: Yak.4:11-12
Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu. Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?

KIITIKIZANO
K. Uniponye roho yangu, maana nimekukosea. (W. Warudie)
K. Nikasema: 'Unihurumie, Ee Bwana.'
W. Maana nimekukosea.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Uniponye...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Moyo wangu wamtukuza Bwana, kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Moyo wangu wamtukuza Bwana, kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo.

MAOMBI
Kristo anataka watu wote waokoke. Tumwombe ili yale anayotaka yatendeke.
W. Uwavutie watu wote kwako, Ee Bwana.

Bwana, kwa kufa kwako msalabani umetukomboa kutoka katika utumwa wa dhambi:
- utuongoze kwenye uhuru na utukufu wa wana wa Mungu. (W.)

Uwaongoze Askofu wetu F..., na maaskofu wote wa Kanisa lako:
- uwajalie ujasiri na huruma katika utumishi wao. (W.)

Uwasaidie wale wanaoutafuta ukweli waupate:
- na waishi kadiri ya ukweli huo. (W.)

Uwapokee ndugu zetu marehemu katika ufalme wa mbinguni,
- ambako wewe, pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, unatawala milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana Mungu, ni wajibu wetu kukutangaza Wewe kuwa ndiwe nuru isiyofifia wala kubadilika: tunapoufikia mwisho wa siku hii utuangaze, na, kwa huruma yako, utusamehe dhambi zetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.