Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 19 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa,
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Nayashika maagizo yako, maana kwa hayo unanihuisha.

Zab.119:89-96 XII Sheria ya Mungu hutegemewa
Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yoh.13:34)

Neno lako, Ee Mungu, ladumu milele;*
limethibitika juu mbinguni.

Uaminifu wako wadumu vizazi vyote,*
umeiweka dunia mahali pake, nayo yadumu.

Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo,*
kwa sababu vyote ni watumishi wako.

Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu,*
ningalikwisha angamia kwa taabu zangu.

Sitasahau kamwe maagizo yako,*
maana kwa hayo umenipa uhai.

Mimi ni wako, unisalimishe,*
maana nimejitahidi kuzishika amri zako.

Waovu wanivizia wapate kuniua;*
lakini mimi nitazitafakari sheria zako.

Nimetambua kila kitu kina mpaka wake,*
lakini agizo lako halina mpaka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nayashika maagizo yako, maana kwa hayo unanihuisha.

ANT. II: Ee Bwana, umekuwa tumaini langu tangu ujana wangu.

Zab.71 Mungu tumaini la wazee
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida (Rom.12:12)

I
Ee Mungu, nimekukimbilia wewe;*
usiniache kamwe niaibike.

Kwa uadilifu wako uniopoe, uniokoe;*
unitegee sikio lako, unisalimishe!

Uwe mwamba wangu wa kukimbilia,/
ngome imara ya kunisalimisha;*
kwani wewe ni mwamba na ngome yangu.

Uniokoe, Ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu;*
uniokoe kutoka kwa wabaya na wakatili.

Maana wewe Bwana u peke yako tegemeo langu,*
Ee Mungu, nimekutumainia tangu ujana wangu;

nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu,/
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu.*
Daima nakusifu wewe.

Kwa wengi nimekuwa mfano wa kushangaza;*
lakini wewe u kimbilio langu imara.

Kinywa changu kimejaa sifa zako,*
na utukufu wako mchana kutwa.

Wakati wa uzee usinitupe;*
niishiwapo na nguvu usiniache.

Maana adui zangu wananisema;*
wanaonivizia wanashauriana,

na kusema: “Mungu amemwacha;/
mfuateni na kumkamata,*
kwani hakuna wa kumwokoa!“

Usikae mbali nami, Ee Mungu;*
uje hima kunisaidia, Ee Mungu wangu.

Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa;*
wenye kunitakia mabaya wapate aibu na dhihaka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, umekuwa tumaini langu tangu ujana wangu.

ANT. III: Ee Mungu, usiniache, hata katika uzee wangu.

II
Lakini mimi nitasubiri kwa tumaini;*
tena nitakusifu zaidi na zaidi.

Mimi nitasimulia matendo yako ya haki,/
nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu;*
ijapokuwa yanapita akili yangu.

Nitaanza na matendo yako makuu, Ee Bwana Mungu*
nitatangaza wema wako peke yako.

Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu*
tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu.

Usiniache, Ee Mungu, hata nikiwa mzee mwenye mvi,*
mpaka nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako.

Uwezo na uadilifu wako, Ee Mungu,*
vimefika mpaka mawinguni.

Wewe umefanya mambo makuu mno.*
Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?

Umeniletea taabu na shida nyingi,*
lakini utanipatia tena uzima na kuniinua.

Utaniongezea heshima yangu,*
na kunifariji tena.

Ndipo nitakusifu kwa kinanda,*
kwa sababu ya uaminifu wako, Ee Mungu wangu;

nitakuimbia sifa kwa kinubi,*
ewe Mtakatifu wa Israeli.

Nitashangilia ninapoimba sifa zako;*
nitaimba kwa moyo wote, maana umeniokoa.

Nitasimulia uadilifu wako mchana kutwa,/
maana walionitakia mabaya,*
wameona aibu na fedheha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Ee Mungu, usiniache, hata katika uzee wangu.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 2Kor.13:11
Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa mapendo na amani atakuwa nanyi.

K. Bwana huwaelekezea macho yake waadilifu.
W. Huwategea sikio wamwombapo.

SALA:
Tuombe: Ee Baba Mwema, Mwumba wa vyote, umewaamuru watu wote kufanya kazi katika ulimwengu wako, na kwa ushirikiano wao, kuinua hali ya binadamu. Utujalie daima tuweze kufanya kazi pamoja kama watoto wa familia yako, na kuwapenda watu wote kidugu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Rom.6:22
Sasa, mmekwisha pewa uhuru kutoka dhambi, na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uzima wa milele.

K. Bwana, tunajua utaturudishia uzima.
W. Ndipo watu wako watakufurahia.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu, Bwana na Mkuu wa ulimwengu wote, unayetupangia kazi na kutupatia mastahili ya kazi zetu. Tunakuomba utusaidie tuweze kuvumilia taabu zote za leo, na kutekeleza kwa furaha matakwa yako katika yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.1:21-22
Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu, na mlikuwa adui zake kwa sababu ya fikra zenu na matendo yenu maovu. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa Watakatifu, safi na bila lawama.

K. Mwimbieni Bwana, enyi watakatifu wake.
W. Msifuni mkikumbuka utakatifu wake.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu, unatualika tusali muda huu ambapo mitume walienda hekaluni kusali. Tunakuomba kwa moyo mnyofu, uwajalie wokovu wote wanaokuomba kwa jina la Yesu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu..

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.