JUMATATU JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Law.19:1-2,11-18
Bwana akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa
watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane
uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana.
Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako
usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu
wako; Mimi ndimi Bwana. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi
mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya watu wako,
kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; Mimi ndimi Bwana. Usimchukie ndugu
yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye
kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako nafsi yako; Mimi
ndimi Bwana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:7-9, 14
1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)
3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele,
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)
4. Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zake, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)
SHANGILIO: Zab.51:1-10,12
Ee Mungu, uniumbie moyo safi; Unirudishie furaha ya wokovu wako.
INJILI: Mt.25:31-46
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika
watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote
watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka
kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko
mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari tangu
kuubwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha;
nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama;
nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona
una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha,
au u uchi, tukakuvika? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo
wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa
kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na
malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa
mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa na kifungoni, msije kunitazama.
Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni,
au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia,
Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia
katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
MAOMBI
Ee Mungu, leo umetukumbusha tena kutimiza Amri Kuu ya Mapendo ili tujiandae vema kwa hukumu yako ya
mwisho. Na hivi twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Utuepushe na majanga ya kudhulumiana mali, ya wizi, unyang'anyi na udanganyifu.
2. Uzuie makwazo na utujalie kipaji cha kuwapatanisha wenzetu kwa hukumu ya haki isiyo na upendeleo wowote.
3. Tunapokosewa na wenzetu utuamshie fadhila ya kutolipa kisasi wala kuwa na kinyongo nao; bali tuwatendee
vile tunavyopenda kutendewa.
4. Kwa huruma yako, usiwahesabie hukumu ndugu zetu marehemu, bali uwakaribishe kwenye makao yako ya milele.
Ee Bwana Mungu, utujalie kukumbuka daima kuwa lolote tulilomtendea mmoja wa ndugu zetu ijapo mdogo
tumekutendea wewe. Basi, utuepushe na laana ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.