Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'

Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.

Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.

ANT. I: Wewe ndiwe nikuombaye, Ee Bwana; asubuhi wanisikia.

Zab.5:1-9,11-13 Sala wakati wa hatari
Wale waliopokea Neno la Mungu ambalo lakaa ndani yao, watafurahi milele.

Ee Mungu, uyasikie maneno yangu;*
uyasikilize malalamiko yangu.

Usikilize kilio changu,/
Ee Mungu, mfalme wangu;*
maana wewe ndiwe nikuombaye.

Ee Mungu, alfajiri waisikia sauti yangu,/
asubuhi nakutolea sadaka yangu,*
kisha nakutazamia.

Wewe si Mungu wa kupenda uovu;*
kwako hawezi kukaa mtu mwovu.

Wenye majivuno hawastahimili mbele yako;*
wewe wawachukia wote watendao maovu.

Wawaangamiza wote wasemao uwongo;*
wawachukia wauaji na wadanganyifu.

Lakini, kwa upendo wako mkuu,*
mimi nitaingia nyumbani mwako;

nitaabudu kwa uchaji,*
katika Hekalu lako takatifu.

Kwa uadilifu wako, Ee Mungu, uniongoze,/
kwa sababu adui zangu ni wengi;*
uiweke njia yako wazi mbele yangu.

Maneno ya adui zangu hayaaminiki,*
nia yao ni kuleta maangamizi;

wanabubujika maneno ya kubembeleza,*
lakini kwa kweli ni maneno ya kuua.

Lakini wote wakukimbiliao wafurahi;*
daima waimbe kwa shangwe.

Uwalinde wanaolipenda jina lako;*
ili wafurahi kwa sababu yako.

Maana wewe Mungu, wambariki mwadilifu;*
kama ngao, wamkinga kwa fadhili yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Wewe ndiwe nikuombaye, Ee Bwana; asubuhi wanisikia.

ANT. II: Ee Bwana, Mungu wetu, twalisifu jina lako tukufu.

WIMBO: 1Nya.39:10-13 Heshima na utukufu viwe kwa Mungu peke yake
Atukuzwe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu kristo (Ef.1:3)

Uhimidiwe, Ee BWANA,/
Mungu wa Israeli baba yetu,*
milele na milele.

Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza,*
na utukufu, na kushinda, na enzi;

maana vitu vyote*
vilivyo mbinguni na duniani ni vyako.

Ufalme ni wako, Ee BWANA,/
nawe umetukuzwa,*
u mkuu juu ya vitu vyote.

Utajiri na heshima hutoka kwako wewe,*
nawe watawala juu ya vyote;

na mkononi mwako mna uweza na nguvu;*
tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.

Basi sasa, Mungu wetu,*
twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, Mungu wetu, twalisifu jina lako tukufu.

ANT. III: Mwabuduni Mungu katika makao yake matakatifu.

Zab.29 Sauti ya Mungu katika dhoruba
Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye" (Mt.3:17)

Msifuni Mungu, enyi viumbe vya mbinguni;*
msifuni Mungu mtukufu na mwenye nguvu.

Lisifuni jina tukufu la Mungu;*
mwabuduni Mungu anapotokea.

Sauti ya Mungu yasikika juu ya maji mengi;/
Mungu mtukufu ananguruma,*
sauti ya Mungu yasikika juu ya bahari!

Sauti ya Mungu ina nguvu,*
sauti ya Mungu imejaa fahari.

Sauti ya Mungu huvunja mierezi;*
naam, hata mierezi ya Lebanoni.

Huifanya milima ya Lebanoni/
irukeruke kama ndama,*
na mlima Hermoni kama mwana-nyati.

Sauti ya Mungu hutoa miali ya moto./
Sauti ya Mungu hutetemesha jangwa;*
Mungu atetemesha jangwa la kadeshi.

Sauti ya Mungu huitikisa mivule;*
hukwanyua majani ya miti msituni,

wakazi Hekaluni mwake wote wasema:*
"Utukufu kwa Mungu!"

Mungu atawala juu ya gharika:*
Mungu ni mfalme, atawala milele.

Mungu atawapa watu wake nguvu:*
atawabariki watu wake na amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mwabuduni Mungu katika makao yake matakatifu.

SOMO: Isa.2:3
Njooni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sion itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu.

KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu wa Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Inua macho yako, Ee Yerusalemu, uone uwezo wa mfalme. Tazama, Mwokozi yu aja. Atakufungulia vifungo vyako.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Inua macho yako, Ee Yerusalemu, uone uwezo wa mfalme. Tazama, Mwokozi yu aja. Atakufungulia vifungo vyako.

MAOMBI
Tuanzapo tena kazi zetu za kila siku, tunamgeukia Kristo na kumwomba baraka zake.
W. Njoo, Bwana Yesu!

Kristo, Nyota ya Mchana, ufukuzaye giza kwa uwezo mkubwa:
- amsha imani yetu. (W.)

Utujulishe kwamba upo duniani,
- kwa njia ya maisha ya Wakristo. (W.)

Njoo, uumbe dunia mpya,
- itakayokuwa na haki na amani. (W.)

Ondoa giza la majivuno yetu,
- na uifanye mioyo yetu iwe minyenyekevu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utujalie neema ili tuwe daima katika kumngoja Kristo, Mwanao. Atakapokuja na kugonga mlangoni petu, atukute tunasali na kutangaza kwa furaha utukufu wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.