JUMATATU JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.
Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.
Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB
ANT. I: Bwana anawatunza wanyonge na wanaoonewa.
Zab.11 Mtumaini Mungu
Mungu ndiye kimbilio langu!/
Mbona mwaniambia:*
"Ruka kama ndege, kimbilia mlimani?
Tazama waovu wanavyovuta upinde;/
wameweka mishale tayari juu ya uta,*
wawapige mshale gizani watu wema.
Kama misingi ikiharibiwa,*
mtu mwadilifu atafanya nini?"
Mungu yumo katika Hekalu lake takatifu;*
kiti cha enzi cha Mungu kiko mbinguni.
Macho yake huwaangalia wanadamu,*
na anajua wanachofanya.
Mungu huwapima waadilifu na waovu;*
huwachukia kabisa watu wakatili.
Atawanyeshea wakosefu makaa ya moto;*
kiberiti na upepo wa hari vitakuwa adhabu yao.
Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu;*
wanyofu watamwona.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Bwana anawatunza wanyonge na wanaoonewa.
ANT. II: Heri wenye moyo safi: maana watamwona Mungu.
Zab.15 Rafiki ya Mungu
Ee Mungu, nani awezaye kukaa hemani mwako?*
nani awezaye kukaa juu ya mlima wako mtakatifu?
Ni mtu anayeishi bila hatia,/
atendaye daima yaliyo sawa,*
asemaye ukweli kutoka moyoni,
na ambaye hasengenyi watu./
Ni mtu ambaye hamtendei ubaya mwenzake,*
wala hamfitini jirani yake.
Mtu huyo huwadharau wafisadi,/
lakini huwaheshimu wamchao Mungu.*
Hutimiza ahadi yake hata kama ikimtia hasara.
Hukopesha bila kutaka faida,/
wala hali rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.*
Mtu mwenye sifa hizo, atakuwa imara milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Heri wenye moyo safi: maana watamwona Mungu.
ANT. III: Mungu alituchagua katika Mwanae, akatufanya tuwe wanawe.
WIMBO: Ef.1:3-10 Azimio la Mungu kuhusu wokovu
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake
katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Mungu alituchagua katika Mwanae, akatufanyatuwe wanawe.
SOMO: Filp.3:20b-21
Twatazamia kwa hamu kubwa Mkombozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili
miili yetu dhaifu inayokufa na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu kwa nguvu ile ambayo
kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya Utawala wake.
KIITIKIZANO
K. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe. (W. Warudie)
K. Utuoneshe uso wa tabasamu, nasi tutakuwa salama.
W. Njoo kwetu, utuokoe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana, Mungu...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Malaika wa Bwana alimpasha Maria habari njema, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Malaika wa Bwana alimpasha Maria habari njema, naye akapata
mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, aleluya.
MAOMBI
Tunapofanya masifu yetu ya jioni, tunakiri kulikuwa na wakati tulipochuchumia giza, na kukataa mwanga halisi.
W. Bwana, tupate kuona!
Ulikuwa mwanadamu, ukaja duniani:
- utuondoe kutoka katika giza la dhambi ya ulimwengu. (W.)
Utusamehe na kutuondolea chuki na wivu, hali ambazo hutuzuia kuona;
- utujalie moyo wa ukarimu. (W.)
Unatujia kwa njia ya wenzetu tunaoishi nao,
- ifungue mioyo yetu tupate kukutambua. (W.)
Bwana, usiwasahau ndugu zetu marehemu,
- ambao walitazamia kuuona mwanga wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana, utujalie neema ili tuwe daima katika kumngoja Kristo, Mwanao. Atakapokuja na kugonga
mlangoni petu, atukute tunasali na kutangaza kwa furaha utukufu wake. Tunaomba hayo kwa njia
ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu,
daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.