Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 20 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tufurahi katika Bwana; na tumsifu kwa nyimbo.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Njoo, ewe Roho Mwumbaji, njoo,
Katika mioyo yetu fanya maskani yako;
Tupe hisani zako za daima,
Sisi tunaoishi na kumudu
Kwa nguvu zako na wako uweza.

Washa mi'li yetu kwa moto wako,
Elekeza tena yetu mioyo
Kwenye upendo wako wa kimungu;
Mi'li yetu ilo dhaifu sana
Hiyo itie nguvu ya kudumu.

Umfukuzie mbali shetani
Alo adui yetu duniani,
Tupate ishi katika amani;
Baya au ovu halitatupata
Wewe ukiwa kiongozi wetu.

Kwa njia yako basi tujifunze,
Tukamjue Baba, pia Mwana,
Na tukakufahamu wewe Roho
Uliyetoka kwa hao wawili,
Ili twabudu kwa imani kweli.

ANT. I: Asubuhi, Bwana, watushibisha kwa pendo lako.

Zab.90 Mungu wa milele na binadamu kiumbe
Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja(2Pet.3:8)

Ee Mungu, tangu awali,*
wewe umekuwa makao yetu.

Kabla ya kuwepo milima,*
kabla hujauumba ulimwengu;

wewe, ndiwe Mungu,*
tangu milele na hata milele.

Ukimwambia binadamu, "Siku zako zimekwisha,"*
binadamu hurudia mavumbini alikotoka!

Kwako miaka elfu ni kama siku moja tu,/
ni kama jana ambayo imekwisha pita;*
kwako ni kama mkesha mmoja tu wa usiku!

Wawafutilia mbali watu kama ndoto!*
Binadamu ni kama nyasi:

asubuhi huchipua na kuchanua,*
jioni zimekwisha nyauka na kukauka.

Hasira yako inatuangamiza;*
tunatishwa na ghadhabu yako.

Maana wewe wayajua maovu yetu;*
wayafichua madhambi yetu kwa mwanga wako.

Kwa hasira yako maisha yetu yatoweka,*
yanaisha kama pumzi.

Huenda tukaishi miaka sabini,*
au tukiwa wenye afya, themanini;

lakini yote ni shida na taabu!*
Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara!

Nani anayetambua uzito wa hasira yako?*
Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako?

Utufundishe ufupi wa maisha yetu,*
ili tuweze kuwa na hekima.

Urudi, Ee Mungu! Utakasirika hata lini?*
Utuonee huruma sisi watumishi wako.

Utujaze upendo wako mkuu asubuhi,*
tushangilie na kufurahi maisha yetu yote.

Utujalie sasa miaka mingi ya furaha,*
kama ulivyotupa miaka mingi ya shida na taabu.

Utuoneshe matendo yako sisi watumishi wako;*
uwaoneshe wazao wetu uwezo wako mtukufu.

Ee Bwana, Mungu wetu, utufadhili;/
utegemeze kazi zetu,*
ufanikishe shughuli zetu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Asubuhi, Bwana, watushibisha kwa pendo lako.

ANT. II: Sifa za Bwana zisikike kutoka miisho ya dunia.

WIMBO: Isa.42:10-16 Wimbo kwa Mungu aliye Mshindi na Mwokozi
Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi (Ufu.14:3)

Mwimbieni BWANA wimbo mpya,*
Na sifa zake tokea mwisho wa dunia;

Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo,*
Na visiwa, nao wakaao humo.

Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao,*
Vijiji vinavyokaliwa na Kedari;

Na waimbe wenyeji wa Sela,*
Wapige kelele toka vilele vya milima.

Na wamtukuze BWANA,*
Na kutangaza sifa zake visiwani.

BWANA atatokea kama shujaa;*
Ataamsha wivu kama mtu wa vita;

Atalia, naam, atapiga kelele;*
Atawatenda adui zake mambo makuu.

Siku nyingi nimenyamaza kimya'*
Nimenyamaza, nikajizuia;

Sasa nitapiga kelele/
Kama mwanamke aliye katika kuzaa;*
Nitaugua na kutweta pamoja.

Nitaharibu milima na vilima,*
Nitavikausha vyote vimeavyo;

Nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa,*
Na kuyakausha maziwa ya maji.

Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua;*
Katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza;

Nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,*
Na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Sifa za Bwana zisikike kutoka miisho ya dunia.

ANT. III: Lisifuni jina la Bwana, ninyi mnaosimama nyumbani mwa Bwana.

Zab.135:1-12 Sifa kwa Mungu
Ninyi ni ukoo mteule, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu (1Pet.2:9)

Lisifuni jina la Mungu,*
enyi watumishi wa Mungu,

mnaosimama nyumbani mwa Mungu,*
Hekaluni mwa Mungu wetu.

Msifuni Mungu kwa kuwa ni mwema;*
liimbieni jina lake sifa, maana inafaa.

Mungu amejichagulia Yakobo kuwa wake,*
watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.

Najua hakika kuwa Mungu ni mkuu;*
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.

Mungu hufanya yote anayotaka,*
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.

Huleta mawingu kutoka mipaka ya dunia;/
hufanya gharika kuu kwa umeme,*
na huvumisha upepo kutoka ghala zake.

Aliwaua wazaliwa wa kwanza kule Misri,*
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.

Alifanya ishara na maajabu kwako, ee Misri,*
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.

Aliyaangamiza mataifa mengi,*
akawaua wafalme wenye nguvu:

akina Sihoni, mfalme wa Waamori,*
na Ogu, mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani.

Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;*
aliwapa Waisraeli ziwe urithi wao.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Lisifuni jina la Bwana, ninyi mnaosimama nyumbani mwa Bwana.

SOMO: Yud.8:26
Yakumbukeni yote aliyomtendea Abrahamu, na majaribu yote aliyomjaribia Isaka, na yote yaliyompata Yakobo katika Mesopotamia ya Shamu alipowachunga kondoo za mjomba wake Labani.

KIITIKIZANO
K. Furahini katika Bwana, enyi waadilifu; kwa maana kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. (W. Warudie)
K. Mwimbieni wimbo mpya.
W. Kwa maana kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Furahini...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Atukuzwe Bwana, kwa kuwa ametujia na kutukomboa.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Atukuzwe Bwana, kwa kuwa ametujia na kutukomboa.

MAOMBI
Baba Mwenyezi, mbingu haziwezi kuushika ukuu wako: hata hivyo, kwa njia ya Mwanao tumejifunza kusema:
W. Baba, utawala wako ufike!

Sisi wanao tunakusifu;
- jina lako litukuzwe katika mioyo ya watu wote. (W.)

Utusaidie leo tuweze kuishi tukiwa na tumaini la kufika mbinguni:
- utufanye tuwe tayari kutekeleza matakwa yako hapa duniani. (W.)

Utupe leo moyo wa kuwasamehe wenzetu,
- kama unavyotusamehe makosa yetu. (W.)

Baba, uwe nasi katika majaribu yetu yote:
- usikubali tutengane nawe. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, uliyewakabidhi wanadamu dunia ili waitumie na kuitunza, na uliyelifanya jua, ili liwaangazie na kuwapa watu mahitaji yao: utujalie leo neema ili tukafanye kazi kiaminifu kwa ajili ya utukufu wako, na kwa ajili ya mahitaji ya jirani zetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.