Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 20 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Twakusifu, Baba, kwa zawadiyo
Ya giza nayo ya jua machweo
Ambayo huonesha kwa mfano
Lile fumbo la kifo liongozalo
Kwenye siku isiyo na muisho.

Mikononi mwako twapumzika;
Tulalapo tutie nguvu mpya;
Wajalie watu wako mioyo
Iamkayo katika upendo
Kwako wewe, Bwana usiyelala.

Na tutafute wako utukufu
Daima, pumzikoni, kazini,
Hadi hapo wake utimilifu
Utakapofunuliwa kabisa
Ee Utatu, chanzo cha uzima.

ANT. I: Mshukuruni Bwana, kwa maana adhili zake ni za milele.

Zab.136 Wimbo wa shukrani
Kuzitangaza kazi za Bwana ni kumsifu Mungu (Cassiodorus)

I
Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Mshukuruni Mungu aliye juu ya miungu yote;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Mshukuruni Bwana aliye juu ya mabwana wote;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Ndiye peke yake atendaye miujiza mikuu;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Kwa hekima yake aliziumba mbingu;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliitengeneza nchi juu ya vilindi vya maji;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliumba jua, mwezi na nyota;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Jua liutawale mchana;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

mwezi na nyota zitawale usiku:*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mshukuruni Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele.

ANT. II: Kazi zako ni kuu na za ajabu, Bwana, Mungu Mwenyezi.

II
Aliwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Akawaondoa watu wa Israeli kule Misri;*
upendo wake mkuu wadumu milele;

kwa mkono wake wa nguvu na enzi;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliigawa bahari ya Shamu;*
upendo wake mkuu wadumu milele;

akawapitisha humo watu wa Israeli;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Akawazamisha humo Farao na jeshi lake;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliwaongoza watu wake jangwani;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliwapiga wafalme wenye nguvu;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Aliwaua wafalme maarufu;*
upendo wake mkuu wadumu milele;

alimwua Sihoni, mfalme wa Waamori,*
upendo wake mkuu wadumu milele;

na Ogu, mfalme wa Bashani;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Alichukua nchi zao akawapa watu wake;*
upendo wake mkuu wadumu milele;

ziwe mali ya Israeli, mtumishi wake;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Alitukumbuka wakati wa unyonge wetu;*
upendo wake mkuu wadumu milele;

akatuokoa na adui zetu;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Hukipa chakula kila kiumbe chenye uhai;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Mshukuruni Mungu wa mbinguni;*
upendo wake mkuu wadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Kazi zako ni kuu na za ajabu, Bwana, Mungu Mwenyezi.

ANT. III: Mungu alikusudia kuvikusanya pamoja viumbe vyote, na kuviweka chini ya Kristo, wakati utimiapo.

WIMBO: Ef.1:3-10 Mungu Mwokozi
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu alikusudia kuvikusanya pamoja viumbe vyote, na kuviweka chini ya Kristo, wakati utimiapo.

SOMO: 1Tes.3:12-13
Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi. Hivyo ataimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu, wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.

KIITIKIZANO
K. Ee Bwana, sala yangu ifike mbele yako. (W. Warudie)
K. Ipande kwako kama moshi wa ubani.
W. Ifike mbele yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ee Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ee Mungu wangu, moyo wangu na utangaze ukuu wako milele.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ee Mungu wangu, moyo wangu na utangaze ukuu wako milele.

MAOMBI
Tumwombe Mungu, ambaye hawaachi kamwe wale wanaomtumainia.
W. Bwana, kwa huruma yako, uzisikie sala zetu.

Ulijalie Kanisa Roho wako;
- uwawezeshe watu kuona wingi wa rehema zako katika Kanisa hilo. (W.)

Uwaongoze mapadre na watumishi wa Kanisa lako:
- uwajalie waweze kuishi kadiri ya mahubiri yao. (W.)

Utufundishe tuweze kuelewana zaidi na zaidi:
- na kwa uwepo wako, utuondolee hofu na hali ya kudhaniana vibaya. (W.)

Uwajalie watu wa ndoa uaminifu na uelewano wa daima:
- shida zao zisiwatenganishe, bali zisaidie kukuza upendo kati yao. (W.)

Uwasamehe dhambi zao ndugu zetu wote waliofariki dunia:
- uwajalie wapate kufurahia maisha mapya, pamoja na watakatifu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Kaa nasi, Bwana Yesu, jioni hii: uwe mwenzi wetu katika njia yetu. Kwa huruma yako, ichochee mioyo yetu na uyaamshe matumaini yetu, ili, tunapounganika na ndugu zetu, tukutambue katika maandiko matakatifu na katika kuumega Mkate. Unayeishi na kutawala na Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.