JUMATATU JUMA 20 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Eze.24:15-24
Neno la Bwana likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako. Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu. Basi nalisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa. Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo. Nikawaambia, Neno la Bwana lilinijia, kusema, Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu. Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe. Basi ndivyo Ezekielii atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Kum.32:18-21(K)18
1. Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa,
Mungu aliyekuzaa umemsahau.
Bwana akaona, akawachukia,
Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.

(K) Umemsahau Mungu aliyekuzaa.

2. Akasema, Nitawaficha uso wangu,
Nitaona mwisho wao utakuwaje;
Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,
Watoto wasio imani ndani yao. (K)

3. Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu;
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu,
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. (K)

SHANGILIO: 1Sam.3:9,Yn.6:68
Aleluya, aleluya!
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!

INJILI: Mt.19:16-22
Mtu mmoja alimwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyonavyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.