JUMATATU JUMA 2 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Dan.9:4-10
Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote uliowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.79:8-9,1,13(K)103:10
1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana.

(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.

2. Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

3. Kuugua kwake aliyefungwa na kuingie mbele zako.
Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

SHANGILIO: Mt.4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

INJILI: Lk.6:36-38
Yesu aliwambia wafuasi wake: Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

MAOMBI
Ee Bwana Mungu Mkuu, sisi watu wako twakiri kuwa tu wakosefu. Tunakushukuru kwa kutupatia Kipindi hiki cha Kwaresima chenye mwaliko wa toba. Na hivi, twakuomba:

Kiitikio: Utuhurumie na utusikilize.
1. Uamshe mioyoni mwetu roho ya toba tupate kukuungamia dhambi zetu.

2. Utupe ari ya kuwasikiliza manabii unaowatuma kutuhubiria neno lako.

3. Utufanye wenye huruma kama wewe ulivyo na huruma.

4. Uwarehemu ndugu zetu marehemu, ili wauone uso wako na kufurahia wokovu wako.

Ee Baba yetu Mwema, tunataka sasa kuwa watoto wako wema wenye kuzitii amri zako. Ubariki nia zetu njema, ili tukayatimize hayo kwa ajili ya wokovu wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.