Generic placeholder image

JUMATATU JUMA LA 34
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tufurahi katika Bwana; na tumsifu kwa nyimbo.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Njoo, ewe Roho Mwumbaji, njoo,
Katika mioyo yetu fanya maskani yako;
Tupe hisani zako za daima,
Sisi tunaoishi na kumudu
Kwa nguvu zako na wako uweza.

Washa mi'li yetu kwa moto wako,
Elekeza tena yetu mioyo
Kwenye upendo wako wa kimungu;
Mi'li yetu ilo dhaifu sana
Hiyo itie nguvu ya kudumu.

Umfukuzie mbali shetani
Alo adui yetu duniani,
Tupate ishi katika amani;
Baya au ovu halitatupata
Wewe ukiwa kiongozi wetu.

Kwa njia yako basi tujifunze,
Tukamjue Baba, pia Mwana,
Na tukakufahamu wewe Roho
Uliyetoka kwa hao wawili,
Ili twabudu kwa imani kweli.

ANT. I: Lini nitaingia, ili niuone uso wa Mungu?

Zab.42 Sala ya mkimbizi
Kisha, ye yote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yo yote (Ufu.22:17)

Kama paa atamanivyo maji ya chemchemi,*
ndivyo nami ninavyokutamani, Ee Mungu wangu!

Nina kiu ya Mungu,/
naam, ya Mungu aliye hai.*
Nitafika kwake lini nakumwona?

Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku;*
kila siku wananiambia: "Yuko wapi basi, Mungu wako?"

Ninasongwa na huzuni nikikumbuka ya awali:*
jinsi nilivyoandamana na umati,

nikiongozana nao kwenda nyumbani kwa Mungu,/
tukipiga vigelegele na kuimba nyimbo za shukrani,*
kati ya umati wa watu wanaofanya sherehe.

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu,*
nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Nimesongwa na huzuni moyoni,*
kwa hiyo ninakukumbuka wewe, Ee Mungu,

kutoka katika nchi ya Yordan na Hermon,*
na kutoka mlima Mizar.

Ameniletea vilindi na maporomoko ya uchungu,*
mawimbi na mafuriko yake yameniangukia.

Mungu hunijalia upendo wake mkuu mchana;/
nami namwimbia wimbo wa sifa usiku,*
ombi kwake yeye anipaye uhai.

Namwambia Mungu, mwamba wangu:*
kwa nini umenisahau?

Mbona naendelea kuhuzunika,*
kwa sababu ya kukandamizwa na adui zangu?

Nimepondwa kwa matukano yao,/
wanaponiulizia kila siku;*
"Yuko wapi basi, Mungu wako?"

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu,*
nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Lini nitaingia, ili niuone uso wa Mungu?

ANT. II: Utuonyeshe, Ee Bwana, mwanga wa huruma yako.

WIMBO: YBS.36:1-5,10-13
Sala ya kuuombea mji mtakatifu Yerusalemu. Na, uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma (Yoh.17:3)

Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe;*
uangalie, uwatishe mataifa yote;

uuinue mkono wako juu ya watu wageni;*
na kuwaonesha nguvu zako zilizo kuu.

Kama vile ulivyojitakasa kati yetu mbele yao,*
Vivyo hivyo ujitukuze kati yao mbele yetu;

nao wakujue Wewe kama sisi tukujuavyo,*
ya kwamba hakuna Mungu ila Wewe peke yako.

Tuoneshe ishara tena,*
na kufanya mambo ya ajabu;

uutukuze mkono wako,*
naam, mkono wako wa kuume.

Uwakusanye kabila zote za Yakobo,/
na kuwafanya urithi wako*
kama siku za kale.

Ee BWANA, uwarehemu/
watu walioitwa kwa jina lako,*
na Israeli uliyemwita mzaliwa wa kwanza wako.

Uuonee huruma/
mji wa patakatifu pako, Yerusalemu,*
mahali pako pa raha;

uujaze Sion adhama yako,*
na patakatifu pako utukufu wako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Utuonyeshe, Ee Bwana, mwanga wa huruma yako.

ANT. III: Utukuzwe, Bwana, katika anga la mbingu.

Zab.19A Utukufu wa Mungu katika viumbe
Mwanga utokao juu umetufikia kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani (Lk.1:79)

Mbingu zadhihirisha utukufu wa Mungu;*
anga laitangaza kazi ya mikono yake.

Mchana waupasha habari mchana ufuatao,*
usiku waufahamisha usiku ufuatao.

Hamna msemo au maneno yanayotumika;*
wala hakuna sauti inayosikika;

hata hivyo, sauti yao yaenea nchini kote;*
ujumbe wao wasikika popote duniani.

Mungu ameliwekea jua makao yake angani;/
nalo latoka nje kama bwana arusi,*
kama shujaa aliye tayari kushindana.

Lachomoza toka upande mmoja,/
na kuzunguka hadi upande mwingine;*
wala hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Utukuzwe, Bwana, katika anga la mbingu.

SOMO: Yer.15:16
Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi.

KIITIKIZANO
K. Furahini katika Bwana, enyi waadilifu; kwa maana kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. (W. Warudie)
K. Mwimbieni wimbo mpya.
W. Kwa maana kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Furahini...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Atukuzwe Bwana, kwa kuwa ametujia na kutukomboa.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Atukuzwe Bwana, kwa kuwa ametujia na kutukomboa.

MAOMBI
Kristo ametushirikisha ukuhani wake. Pamoja naye tunaomba na kutolea nafsi zetu.
W. Bwana, pokea mapendo yetu na utumishi wetu.

Yesu Kristo, wewe ndiwe Kuhani wa milele:
- yatakatifuze matoleo yetu, ili yakubaliwe na Baba. (W.)

Bwana, wewe ndiwe upendo wenyewe:
- utujalie tuweze kukupenda. (W.)

Utupe leo vipaji vya Roho Mtakatifu:
- utufanye tuwe wavumilivu, wema na watulivu. (W.)

Utujalie tuweze kutambua mahitaji ya jirani zetu:
- na utupe moyo wa kuwapenda kindugu. (W.)


Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, Mungu Mwenyezi, utulinde siku nzima ya leo kwa uwezo wako. Vile ulivyotuwezesha kuianza siku hii, usituachilie tugeukie dhambi, bali kwa mawazo, maneno na matendo yetu yote, tukusudie kutenda yale yanayopendeza machoni pako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.