JUMATATU JUMA LA 34
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
ANT. I: Wenye heri wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.
Zab.119:41-48 VI Kutegemea sheria ya Mungu
Unifadhili upendo wako mkuu, Ee Mungu*
uniokoe kama ulivyoahidi.
Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana,*
maana mimi nina imani na neno lako.
Unijalie kusema ukweli daima,*
maana tumaini langu liko katika hukumu zako.
Nitatii sheria yako daima,*
milele na milele.
Nitaishi katika uhuru kamili,*
maana nayatia maanani mafundisho yako.
Nitawatangazia wafalme maagizo yako,*
wala sitaona aibu.
Furaha yangu ni kuzitii amri zako,*
kwa sababu ninazipenda.
Naziheshimu na kuzipenda amri zako;*
nitazitafakari kanuni zako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Wenye heri wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.
ANT. II: Chakula changu ni kutekeleza matakwa ya Baba yangu.
Zab.40:1-13,16-17 Utenzi wa sifa
Hukutaka sadaka wala dhabihu, lakini umenitayarishia mwili (Ebr.10:5)
I
Nilimngojea Mungu kwa uvumilivu,*
akanielekea, na kunisikiliza kilio changu.
Aliniondoa katika shimo la hatari,*
katika matope ya dimbwi,
akaniweka salama juu ya mwamba,*
na kuuimarisha mwenendo wangu.
Alinifundisha wimbo mpya,*
wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa,*
kisha watamtumainia Mungu.
Heri mtu anayemtumainia Mungu;/
mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno,*
waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uwongo.
Ee Mungu, Mungu wangu,*
umetufanyia mambo mengi ya ajabu,
na mipango yako juu yetu haihesabiki;*
hakuna yeyote aliye kama wewe.
Kama ningeweza kusimulia hayo yote,*
idadi yake ingenishinda.
Sadaka na dhabihu hutaki;/
wala hutaki sadaka za kuteketezwa,*
ila umenipa masikio nikusikie.
Ndiyo maana nilisema;/
"Niko tayari, Ee Mungu wangu, kutimiza mapenzi yako,*
kama nilivyoandikiwa katika kitabu cha sheria.
Naufurahia mwongozo wako,*
na kuuzingatia kwa moyo wote."
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Chakula changu ni kutekeleza matakwa ya Baba yangu.
ANT. III: Ingawa mimi ni fukara na mtu wa huzuni, Bwana atanitunza.
II Sala ya kuomba msaada
Mbele ya jumuiya kubwa ya watu,/
nimesimulia habari njema ya ukombozi.*
Wajua, Ee Mungu, kuwa sikunyamaza hata kidogo.
Sikuificha habari hii moyoni mwangu,*
ya kwamba umeniokoa.
Nimetangaza daima uaminifu wako na msaada wako./
Sikuifichia jumuiya kubwa ya watu,*
uaminifu na upendo wako mkuu.
Ee Mungu, usinikatalie huruma yako:/
Upendo wako mkuu na uaminifu wako,*
viniweke salama salimini.
Maafa yasiyohesabika yanizunguka,*
maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona;
ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu,*
nami nimevunjika moyo.
Ee Mungu, upende kuniokoa;*
Ee Mungu, uje sasa kunisaidia.
Lakini wanaokutafuta wewe,*
wafurahi na kushangilia.
Wale wapendao wokovu utokao kwako,*
waseme daima: “Mkuu ni Mungu!”
Mimi ni maskini na fukara, Ee Bwana;*
lakini wewe hukunisahau.
Wewe ni mwokozi wangu na msaada wangu;*
uje, Ee Mungu wangu, usikawie!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Ingawa mimi ni fukara na mtu wa huzuni, Bwana atanitunza.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Yer.31:33
Agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA;
Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
K. Uniumbie moyo ulio thabiti, Ee Mungu.
W. Usinitupe mbali nawe.
SALA:
Tuombe: Ee Baba Mwema, Mwumba wa vyote, umewaamuru watu wote kufanya kazi katika ulimwengu wako,
na kwa ushirikiano wao, kuinua hali ya binadamu. Utujalie daima tuweze kufanya kazi pamoja
kama watoto wa familia yako, na kuwapenda watu wote kidugu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Adhuhuri: Yer.32:40
Nami nitafanya agano la milele pamoja nao; kwamba sitageuka wala kuwaacha, ili niwatendee
mema; nami nitatia kicho changu mioyoni mwao, ili wasiniache.
K. Mungu ni nguvu na wokovu wangu.
W. Yeye ni kimbilio langu.
SALA:
Tuombe: Ee Mungu, Bwana na Mkuu wa ulimwengu wote, unayetupangia kazi na kutupatia mastahili ya
kazi zetu. Tunakuomba utusaidie tuweze kuvumilia taabu zote za leo, na kutekeleza kwa
furaha matakwa yako katika yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Eze.34:31
Na ninyi, kondoo zangu, kondoo za malisho yangu, ni wanadamu, na mimi ni Mungu wenu,
asema Bwana MUNGU.
K. Bwana ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
W. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza.
SALA:
Tuombe: Ee Mungu, unatualika kusali muda huu ambapo mitume walienda hekaluni kusali. Tunakuomba
kwa moyo mnyofu, uwajalie wokovu wote wanaokuomba kwa jina la Yesu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.