JUMATATU JUMA 3 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: 2Fal.5:1-15
Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena likuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi. Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami. Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sana kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema. Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakisema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; naye nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.42:1-2,43:3-4
1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.

(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu.

2. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)

3. Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
Na hata maskani yako. (K)

4. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu. (K)

SHANGILIO: Yn.8:12
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.

INJILI: Lk.4:24-30
Yesu alifika Nazareti akawaambia makutano hekaluni: Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakazwa ila Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipiita katikati yao, akaenda zake.

MAOMBI
Ndugu zangu, wengi tunayo matatizo mengi na makubwa. Huenda mengine yakawa ni ya kuogopwa kama ukoma. Imani thabiti na huruma ya Mungu vyahitajika tupate kuondokana nayo. Ee Bwana Mungu twakuomba:

Kiitikio: Kwa huruma yako, utusikie.
1. Katika mfungo huu wa Kwaresima, wahubiri wote wa neno lako wasikate tamaa kwa kutosikilizwa na watu wasiokujua wewe uliye Mungu wa kweli.

2. Watawala wote wa dunia wasisite kuwapa uhuru wa dini watu wote wanaomtafuta Mungu kwa moyo mnyofu.

3. Ufungue mioyo yetu, ili kila mmnoja wetu ayatambue mapungufu yake na awe tayari kujirekebisha kadiri ya miongozo ya Mama Kanisa.

4. Utujalie imani thabiti juu ya Sakramenti ya Upatanisho ili, kwa huruma yako, tuweze kuziungama dhambi zetu, kuoshwa udhaifu wetu, kuyafuata mashauri ya Injili na kupata wokovu.

Ee Mungu, Mwanao alivumilia mateso mengi ili apate kutukomboa sisi wakosefu. Utujalie kuiga mfano wake ili tuwe manabii jasiri wa ukweli wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.